Sudan: Wawakilishi wa pande hasimu za kijeshi wanakutana nchini Saudi Arabia
NAIROBI – Saudi Arabia itakuwa mwenyeji wa mazungumzo ya kwanza ya ana kwa ana leo Jumamosi kati ya makundi mawili ya kijeshi yanayopigana nchini Sudan wakati huu mapigano yakiendelea kuripotiwa nchini humo licha ya kuwepo kwa wito wa kusitishwa.
Imechapishwa:
Hatua hii ya Saudi Arabia inakuja wakati huu pia makubaliano ya awali yalioafikiwa na pande hizo hasimu za kijeshi ya kusitisha mapigano yakionekana kutibuka kwa mara kadhaa.
Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja kutoka kwa nchi za Marekani na Saudia Arabia imeeleza kuwa kukaribisha kile imetaja kuwa majadiliano ya kabla ya mazungumzo huko Jeddah kati ya jeshi la Sudan na vikosi maalum vya RSF.
Mkutano huu wa kujaribu kupata suluhu ya kinachoendelea nchini Sudan unakuja wakati mapigano yakiendelea kuripotiwa katika baadhi ya miji nchini humo ikiwemo jiji kuu la Khartoum.
Kwa mujibu wa jeshi la Sudan, mazungumzo hayo yanalenga masula muhimu yanayoibuka haswa suala la kibinadamu. Idadi kubwa ya raia jijini Sudan wameendelea kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa chakula na maji kutokana na mapigano hayo.
Wengi wa raia wa Khartoum wameeleza kukabiliwa na changamoto hizo, wakisema kuwa hawawezi kutoka nje kwenda kutafuta bidhaa hizo muhimu kwa kuhofia kushambulia.
Tayari jeshi la Sudan limethibitisha kuwatuma wajumbe wake mjini Jeddah kushiriki katika mazungumzo hayo, japokuwa vikosi vya RSF kwa upande wake havijatoa taarifa yoyote kuhusu suala hili.
Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada yamekuwa yamekuwa yakieeleza kuwa huenda raia nchini humo wakakabiliwa na mzozo wa kibindamu iwapo mapigano hayo yataendelea.
Watu zaidi ya mia nne wamethibitishwa kufariki katika mapigano hayo ya wiki tatu, wengine zaidi ya laki nne wakiripotiwa kuyakimbia makazi yao.
Mataifa jirani na Sudan kama vile Chad na Sudan kusini yameripoti kuwapokea mamia ya raia wa Sudan wanaokimbilia katika mataifa hayo kutafuta hifadhi.