Pata taarifa kuu
MAPIGANO - SUDAN

Sudan: Burhan apuuzilia mbali mazungumzo ili kusitisha mapigano

NAIROBI – Nchini Sudan, milio ya risasi imeendelea kusikika jijini Khartoum, katika siku ya sita ya makabiliano kati ya wanajeshi wa serikali na wapiganaji wa kikosi cha RSF, bila dalili ya kusitishwa kwa vita hivyo.

Raia wanajaribu kuondoka Khartoum huku kukiwa na mzozo kati ya vikosi viwili hasimu vinavyoongozwa na majenerali wa Sudan. (19/04/2023)
Raia wanajaribu kuondoka Khartoum huku kukiwa na mzozo kati ya vikosi viwili hasimu vinavyoongozwa na majenerali wa Sudan. (19/04/2023) REUTERS - EL TAYEB SIDDIG
Matangazo ya kibiashara

Wakati mapigano hayo yakiendelea, idadi ya watu waliopoteza maisha imeendelea kuongezeka, Aprili 20, watu zaidi ya 300 wameripotiwa kupoteza maisha kwa mujibu wa Shirika la afya duniani, WHO.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na watoto UNICEF linasema miongoni mwa watu waliouawa ni watoto, huku Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International likisema, kuna wasiwasi mkubwa wa vita hivyo kuwaathiri wakaazi wa Darfur.

Maelfu ya watu wameshuhudiwa pia wakiukimbia mji huo, kuelekea katika majimbo ambayo yana utulivu, wakati huu mapigano yakiingia siku ya sita.

Nalo shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, limesema watu laki mbili wamekimbia mapigano hayo na kutafuta hifadhi nchini Chad, wengi wao wakiwa wanawake na watoto ambao walikosa bidhaa za kimsingi kama chakula, maji na kinga. 

Majenerali wapimana nguvu 

Kwa mara nyingine pande hizo mbili zilishindwa kuheshimu makubaliano ya kusitisha vita, licha ya kuwepo kwa wito wa Kimataifa, huku makabiliano makali yakiendelea kushuhudiwa katika uwanja wa ndege na makao makuu ya jeshi jijini Khartoum.

Mkuu wa kikosi cha RSF Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, ameimbia Televisheni ya Aljazeera kuwa yupo tayari kusitisha mapigano kipindi cha sikukuu ya Eid.

RSF, kikosi chenye nguvu kilichoundwa kutoka kwa wanachama wa wanamgambo wa Janjaweed ambao waliongoza miaka mingi ya ghasia zilizokithiri huko Darfur, kilisema vikosi vyake "vitajitolea kikamilifu kusitisha mapigano" kuanzia Jumatano jioni kwa saa 24, kama vile jeshi lilivyofanya.

Lakini walioshuhudia walisema milio ya risasi haikukoma Khartoum, kwani usitishaji mapigano mwingine ulikiukwa ndani ya dakika chache baada ya kuanza kwake kwa mara ya pili ndani ya siku nyingi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.