Pata taarifa kuu

China yaunga mkono uwakilishi bora wa Afrika katika Umoja wa Mataifa

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Qin Gang amehudhuria hafla ya uzinduzi wa makao makuu ya Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa kinachofadhiliwa na Beijing katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Qin Gang
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Qin Gang AP - Elizabeth Dalziel
Matangazo ya kibiashara

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Qin Gang amesema siku ya Jumatano kuwa Afrika inapaswa kuwakilishwa vyema katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa baada ya kukutana na mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.

"Tunapaswa kuimarisha uwakilishi na sauti ya nchi zinazoendelea, hasa zile za Afrika, katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa," amesema waziri huyo wakati wa uzinduzi wa makao makuu ya Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Afrika, kilichofadhiliwa na Beijing, mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia.

Qin Gang ametoa wito wa "mfumo wa haki na usawa zaidi wa utawala wa kimataifa", akisema "Afrika inapaswa kuwa njia panda ya ushirikiano wa kimataifa, sio msingi wa ushindani mkubwa wa mamlaka".

"Bara la Afrika halijajumuishwa katika utawala wa kimataifa, na hiyo si haki," ameongeza mwenyekiti wa Tume ya AU, Moussa Mahamat Faki. "Kwa miongo kadhaa sasa tumekuwa tukipigania mageuzi ya mfumo wa kimataifa kwa ujumla na hasa kwa niaba ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa".

"Afrika inakataa kuchukuliwa kama uwanja wa mapambano ya ushawishi", pia amebainisha Moussa Mahamat Faki. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaundwa na wanachama 15, wakiwemo wanachama watano wa kudumu wenye haki ya kura ya turufu: Marekani, Urusi, China, Ufaransa na Uingereza. Nchi nyingine kumi zinakalia viti vingine kwa muda wa miaka miwili.

Waziri wa China yuko katika ziara ya wiki moja barani Afrika, ambayo inapaswa pia kumpeleka Gabon, Angola, Benin na Misri. Nchini Ethiopia, alikutana na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Abiy Ahmed siku ya Jumanne.

Mwezi Septemba mwaka jana, Rais wa Marekani Joe Biden alisema nchi yake itaunga mkono ugawaji wa viti vya kudumu kwa Afrika na Amerika Kusini, pamoja na uungaji mkono wake wa awali wa kujumuishwa kwa Japan na India.

Bwana Biden pia aliunga mkono jukumu la kudumu la AU katika kundi la nchi zilizostawi kiuchumi G20 na anapanga ziara Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambayo itakuwa ni ziara ya kwanza kufanywa na rais wa Marekani tangu 2015.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.