Pata taarifa kuu
DRC- SUDAN KUSINI- USALAMA

Wanajeshi 750 wa Sudan Kusini kwenda Mashariki ya DRC Kujiunga na Jeshi la EAC

Sudan Kusini, inatuma wanajeshi wake 750 kwenda Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kuungana na wanajeshi wengine kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika, zinazounda kikosi cha pamoja, kusaidia kukabiliana na makundi ya waasi.Mengi zaidi na Mwandishi wetu wa Masuala ya Sudan, James Shimanyula

Wanajeshi wa Sudan Kusini
Wanajeshi wa Sudan Kusini AFP - SAMIR BOL
Matangazo ya kibiashara

Wanajeshi hao wa Sudan Kusini wanatarajiwa Mashariki mwa DRC, baada ya kuagwa na rais Salva Kiir jijini Juba, ambaye amewaambia waende wasaidie kuleta amani na kuwalinda raia wa nchi hiyo jirani.

"Nendeni katika Jamhuri ya watu wa Congo, kama wanajeshi wenye nidhamu. Nendeni mkarejeshe hali ya utulivu na wala si kuvizia wanawake na wasichana. Kamwe msifanye hivyo. Msithubutu kuchukua mali ya watu. Wasaidieni raia wakati wanapokuwa mashakani. Lindieni raia na mali yao. Mtakuwa Congo kama wanajeshi wa Sudan kusini." amesema rais Salva Kiir.

Hata hivyo, hatua hii haijaungwa mkono na wadau mbalimbali nchini Sudan Kusini, wanaosema ni aibu kwa jeshi hilo kuondoka nchini, wakati taiafa hilo likiendelea kukabiliwa na tatizo la utovu wa usalama wa mara kwa mara, kama anavyoeleza Alex Kuol  mchambuzi wa masuala ya usalama nchini humo.

"Kamwe sikubaliani na kuchaguliwa kwa kikosi ambacho kimepewa jukumu gumu la kulinda amani kutokana na sababu kwamba wananchi wa Sudan kusini wangali katika kambi za wakimbizi wa ndani.  Hata wanajeshi wengine wanakufa. Nchi yetu haina amani. Inawezezekanaje wanajeshi wetu kwenda nchi nyingine kulinda amani." ameeleza Alex Kuol.

Garang Thon ni mwanaharakati nchini humo naye anasema, Jeshi la Sudan Kusini lina changamoto nyingi, na haamini iwapo uwepo kwao nchini DRC, utasaidia.

"Sidhani kwamba jeshi letu lina ujuzi wa kutosha kupambana na waasi. Wanajeshi wetu wamechoka, Wanajeshi wetu wana njaa na hawafai kushiriki katika mapambano makali." amesisitiza Garang Thon.

Wanajeshi wa Sudan Kusini, wanaugana na wenzao kutoka Kenya, Burundi na Uganda ambao tayari wapo Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kusaidia kuleta utulivu Mashariki mwa nchi hiyo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.