Pata taarifa kuu

Mazungumzo ya amani yanayojumuisha makundi mbalimbali na serikali ya DRC yaanza Nairobi

Awamu nyingine ya mazungumzo ya amani kati ya makundi ya waasi na serikali ya DRC, yameanza leo mchana jijini Nairobi nchini Kenya, na kuhudhuriwa na rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta. Hata hivyo, waasi wa  M23 hawajaalikwa kwenye mazungumzo hayo. 

Mji mkuu wa Kenya, Nairobi ambapo yanafanyika mazungumzo ya amani kati ya serikali ya DRC na makundi yenye silaha.
Mji mkuu wa Kenya, Nairobi ambapo yanafanyika mazungumzo ya amani kati ya serikali ya DRC na makundi yenye silaha. AFP - SIMON MAINA
Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo ndio inaratibu mazungumzo haya ya Nairobi, lengo kubwa ni kuharakisha juhudi za ukanda zinazoendelea ili kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana mashariki mwa DRC. 

Mazungumzo haya yanaenda kufanyika baada ya kuahirishwa juma moja lililopita kupisha mazungumzo yaliyofanyika jijini Luanda, Angola, ambapo viongozi walikubaliana masuala kadhaa ikiwemo, usitishaji wa mapigani, kusalilisha silaha na mazungumzo ya Nairobi kuanza. 

Mazungumzo haya yanafanyika chini ya usimamizi wa rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ambaye akiwa madarakani ndie alieanzisha mchakato huu. 

Siku chache kabla ya mkutano wa Angola, ofisi ya Kenyatta, ilitoa taarifa kuthibitisha mpango wa mazungumzo haya baada ya ziara yake mashariki mwa kongo, ambapo alizitaka pande zinazohasimiana kuweka silaha chini na kuruhusu mazungumzo kuchukua nafasi. 

Ikiwa mazungumzo haya yatafanyika kama yalivyopangwa, itakuwa ni hatua muhimu kuelekea kupata amani ya kudumu, ambapo tayari makundi ya waasi 18 kutoka mashariki mwa nchi hiyo yamethibitisha kushiriki. 

Hata hivyo haijafahamika hadi sasa ikiwa waasi wa M23 watashiriki kutokana na msimamo wa Serikali ya Kinshasa ambayo inawataja waasi hao kama magaidi. 

Hata hivyo wataalamu wameonya kuhusu mazungumzo hayo kutokuwa jumuishi, kutokana na ukweli kuwa kuna makundi zaidi ya 120 yanayotekeleza uhalifu mashariki mwa Kongo. 

Haya yakijiri, kwa siku ya pili mfululizo hivi leo, hali ya utulivu imeshuhudiwa mashariki mwa nchi hiyo, tangu kundi la M23 liseme liko tayari kwa mazungumzo na kufuata maagizo ya viongozi wa nchi za ukanda.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.