Pata taarifa kuu

Dunia yaomboleza kifo cha Askofu Desmond Tutu

Askofu mstaafu wa kanisa Anglikana, Mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu na mtu aliyeshiriki kikamilifu kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, Desmond Tutu, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 90, amethibitisha rais wa Cyril Ramaphosa.

Askofu Desmond Tutu, alikuwa kinara wa kupinga vitendo vya kibaguzi.
Askofu Desmond Tutu, alikuwa kinara wa kupinga vitendo vya kibaguzi. RODGER BOSCH AFP/File
Matangazo ya kibiashara

Askofu Tutu, mmoja ya watu ambao msimamo wao haukutetereka wakati wa vita dhidi ya ubaguzi wa rangi, alifanya kazi kwa nguvu kuhakikisha utawala wa kibaguzi unamalizika nchini Afrika Kusini.

Kiongozi huyu wa kidini ambaye alikuwa askofu wa kwanza mweusi wa Johannesburg na baadae kwenye jiji la Cape Town, alikuwa pia muhamasishaji mkubwa wa maandamano kupinga vitendo vya ubaguzi kwenye taifa hilo.

Akitoa taarifa ya kifo chake, rais Ramaphosa, amesema taifa limepata pigo jingine, kwa kumpoteza mmoja ya watu waliopigania usawa na haki kwenye taifa hilo.

Viongozi mbalimbali wa dunia, akiwemo mtoto wa marehemi Martin Luther King, Bernice King, alimuelezea Askofu Tutu kama mtu jasiri na shudaa kuwahi kutokea katika sayari ya dunia.

Naibu waziri mkuu wa Uingereza, Dominic Raab, amemtaja Tutu kama “Nembo ya dunia”.

Askofu Tutu hapa ilikuwa tarehe 17 Desemba 2021.
Askofu Tutu hapa ilikuwa tarehe 17 Desemba 2021. RODGER BOSCH AFP/Archivos

Aghalabu askofu Tutu amekuwa akipelekwa hospitalini tangu mwaka 2015, baada ya kuwa amethibitishwa kuwa na saratani ya kibofu mwaka 1997.

 

Miaka ya hivi karibuni, Tutu na mke wake wamekuwa wakiishi katika makazi maalumu ya wazee nje ya jiji la Cape Town.

Desmond Mpilo Tutu, alizaliwa Octoba 7 mwaka 1931, katika eneo la Klerksdorp jijini Johannesburg, na baadae akawa mwalimu kabla ya kujiunga na chuo cha Thiolojia mjini Rosetenville mwaka 1958.

Baada ya hapo akawa mchungaji na mwenyekiti wa baraza la makanisa nchini Afrika Kusini kwenye mji wa Lesotho. Mwaka 1985 alitangazwa kuwa askofu wa kwanza mweusi wa kanisa Anglikana mjini Johannesburg na mwaka 1986 akawa askofu wa kanisa hilo mjini Cape Town.

Anasifika pakubwa kuruhusu wanawake kuwa wachungaji pamoja na kuunga mkono haki za watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Mwaka 1980, Tutu alikamatwa kwa kushiriki maandamano na baadae pasi yake ya kusafiri kuzuiliwa kwa mara ya kwanza. Alirejeshewa pasi yake ya kusafiria wakati alipoenda nchini Marekani na bara Ulaya, ambako alifanya mazungumzo na katibu mkuu wa umoja wa Mataifa, kiongozi wa kanisa katoli pamoja na viongozi wengine wa makanisa.

Askofu Tutu alikuwa mcheshi na mtu wa utani mara nyingi anapohutubia.
Askofu Tutu alikuwa mcheshi na mtu wa utani mara nyingi anapohutubia. RODGER BOSCH AFP/File

Katika kipindi ya miaka ya 80, ambapo Afrika Kusini ilikuwa inashuhudia vurugu za kupinga ubaguzi wa rangi pamoja na hali ya dharura iliyokuwa imetangazwa huku jeshi likishika hatamu ya utawala, Tutu alikuwa mtu wa kwanza mweusi kuzungumza hadhari akipinga ubaguzi.

 

Mwaka 1984, Tutu alizawadia tuzo mashuhuri duniani ya mshindi wa Nobel, akitajwa kama mmoja ya watu waliokuwa vinara kupigania haki za binadamu, jambo alilolifanya maisha yake yote.

Wakati utawala wa ubaguzi wa rangi unamalizika nchini Afrika Kusini mwaka 1994, Tutu alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzoni kuunga mkono jamii yenye usawa, akiliita taifa hilo kama “Upinde wa mvua”.

Akipewa jina la utani kama “the Arch”, Tutu alikuwa mcheshi, na kuwa nembo ya taifa lake na historia ya taifa hilo, akifananisha sana na aliyekuwa rafiki yake wa muda mrefu, rais wa kwanza mweusi wa taifa hilo, marehemu, Nelson Mandela.

Mwaka 1990, baada ya miaka 27 gerezani, Mandela alitumia uhuru wake wa mwanzoni katika makazi ya Tutu mjini Cape Town, ambapo baadae Mandela alimtaja Tutu kama “Askofu wa Watu”.

Alipotangazwa kuwa rais mwaka 1994, Mandela alimteua Tutu kuwa mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya Maridhiano na Amani, tume ambayo ilibaini vitendo vingi vya ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi.

Askofu Tutu alishiriki kampeni za kimataifa za ulinzi wa haki za binadamu, hasa haki za watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

“Sitamuabudu Mungu ambaye ni mbaguzi na hivi ndivyo ambavyo binafsi najisikia,” alisema askofu Tutu mwaka 2013 wakati akizindua kampeni ya kutetea watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
“Nitapinga ubaguzui hata nikifika mbinguni. Hapana, nitasema, samahani bora niende ile sehemu nyingine.”

Matamshi yake makali aliyokuwa akiyatoa baada ya kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi, mara kadhaa yalikuwa yakiwaudhi hata washirika wake waliokuwa wakimtuhumu kwa upendeleo.

 

Mwaka 2015, Tutu alifanya kumbukizi ya ndoa yake na mkewe Leah, akikumbuka kiapo cha mwaka 1955.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.