Pata taarifa kuu
RWANDA-HAKI

Mpinzani wa Rwanda ahukumiwa kifungo cha miaka 7 jela kwa matamshi yake Youtube

Mpinzani wa Rwanda ambaye alitumia chaneli yake ya YouTube kuikosoa serikali amehukumiwa kifungo cha miaka saba jela na mahakama ya Kigali, duru za kuaminika zimebaini.

Niyonsenga, anayejulikana zaidi kama Cyuma (kwa kinyarwanda), neno ambalo linamaanisha "chuma," kwenye YouTube, alijulikana kwa video zake akilaani ukiukaji wa haki za binadamu.
Niyonsenga, anayejulikana zaidi kama Cyuma (kwa kinyarwanda), neno ambalo linamaanisha "chuma," kwenye YouTube, alijulikana kwa video zake akilaani ukiukaji wa haki za binadamu. Eric PIERMONT AFP/File
Matangazo ya kibiashara

Dieudonné Niyonsenga, ambaye chaneli yake ya YouTube ya Ishema TV ilikusanya maoni zaidi ya milioni 15, alipatikana na hatia ya makosa manne, ikiwa ni pamoja na kughushi na wizi wa utambulisho.

"Mahakama inazingatia kwamba makosa ambayo Niyonsenga anashtakiwa yalitekelezwa kwa makusudi," amesema jaji, akitoa uamuzi huo siku ya Alhamisi na kulipa faini ya faranga za Rwanda milioni tano (euro 4,280). "Mahakama inaamuru kwamba Dieudonné Niyonsenga akamatwe mara moja na kupelekwa kutumikia kifungo chake gerezani."

"Tunakata rufaa dhidi ya uamuzi huu (...) Sio kisheria," amesema wakili wake Gatera Gashabana siku ya Ijumaa.

Niyonsenga akamatwa nyumbani kwake

Nyota huyo wa YouTube hakufika mahakamani na alikamatwa nyumbani kwake muda mfupi baada ya kesi hiyo.

"Dieudonné Niyonsenga alikamatwa jana katika utekelezaji wa uamuzi wa mahakama. Anajianda kufikishwa jela, Thiery Murangira, msemaji wa polisi ya Rwanda, ameliambia shirika la habari la AFP.

Niyonsenga, anayejulikana zaidi kama Cyuma (kwa kinyarwanda), neno ambalo linamaanisha "chuma," kwenye YouTube, alijulikana kwa video zake akilaani ukiukaji wa haki za binadamu.

Waandesha mashitaka wakata rufaa baada ya kuachiliwa kwake

Mnamo Aprili 2020, alitoa msururu wa video akiwashutumu wanajeshi wa Rwanda kwa unyanyasaji mkubwa dhidi ya wakaazi wa makazi duni, kama sehemu ya vizuizi vikali vilivyowekwa kupambana na janga la corona.

Muda mfupi baadaye, alikamatwa na kushtakiwa kwa kukiuka hatua za kizuizi kwa kujifanya mwandishi wa habari, kabla ya kupelekwa gerezani.

Alifutiwa mashitaka na kuachiliwa miezi 11 baadaye, lakini waendesha mashtaka walikata rufaa.

Rwanda, inayoongozwa na Paul Kagame tangu mwisho wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 ambapo watu 800,000 waliuawa, kulingana na Umoja wa Mataifa, mara kwa mara inashutumiwa na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kukandamiza uhuru wa kujieleza, ukosoaji na upinzani wa kisiasa.

HRW yainyooshea Rwanda kidole cha lawama

Mnamo Machi, shirika la kimataifa la Haki za Binadamu la Human Rights Watch lilionyesha wasiwasi wake juu ya mtazamo wa mamlaka dhidi ya watu wanaotumia YouTube au blogi kuzungumza juu ya masuala yenye utata.

Kulingana na HRW, angalau watu wanane wanaoripoti au kutoa maoni yao kuhusu habari - ikiwa ni pamoja na athari za hatua kali za kupambana na Covid ambazo zimewakumba maskini zaidi - walikuwa wametishwa, kukamatwa au kufunguliwa mashtaka mwaka uliopita.

Mwezi Oktoba, Yvonne Idamange, mama wa watoto wanne, alihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela kwa kuchochea vurugu mtandaoni.

Aimable Karasira, profesa wa chuo kikuu anayejulikana kwa chaneli yake ya YouTube, pia alikamatwa mwezi Juni na kushtakiwa kwa kukana, uhalifu mkubwa nchini Rwanda. Alikishutumu chama cha Paul Kagame cha Rwandan Patriotic Front kwa kukiuka haki za binadamu.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.