Algeria: Imefuta Leseni ya Uendeshaji wa kituo cha Ufaransa ya 24
Serikali ya Algeria imesitisha leseni ya Televisheni ya Ufaransa France 24, siku moja baada ya uchaguzi wa wabunge, ambao wananchi wa taifa hilo la Afrika Kaskazini, wanasubiri matokeo.
Imechapishwa:
Wizara ya Habari nchini humo imesema kuwa, imechukua hatua hiyo kwa kile inachoeleza kuwa, kituo hicho kimeendelea kushambulia taasisi za nchi hiyo.
Tangu tarehe 13 mwezi Machi France 24 ilipokea onyo kutoka kwa serikali ya Algeria baada ya kupeperusha mandamano dhidi ya serikali ya taifa hilo la Afrika Kaskazini.
Hatua hii ya serikali ya Algeria, haijajibiwa na uongozi wa France 24 lakini mwezi Machi, Mkurugenzi Mkuu wa kituo hicho Marc Saikali, alisema kuwa Televisheni hiyo ilikuwa inafanya kazi yake ya uanahabari kwa kuheshimu sheria za nchi hiyo.
Serikali ya Ufaransa ambayo pia imekuwa na uhusiano baridi na Algeria, haijazungumzia kitendo hicho cha serikali ya Algers,wakati huu serikali nchini humo ikiendelea kushutumiwa kuwahangaisha wanahabari wa nje na ndani.