Pata taarifa kuu
AFRIKA KUSINI-RWANDA-HAKI

Afrika Kusini yatoa waranti kwa washtumiwa wa mauaji ya Karegeya

Mahakama nchini Afrika Kusini imetoa waranti za kukamatwa kwa wahusika wakuu wa mauaji ya aliye kuwa mkuu wa idara ya ujasusi nchini Rwanda Patrick Karegeya.

Patrick Karegeya, mkuu wa zamani wa idara ya ujasusi ya Rwanda, alizikwa Johannesburg Januari 19, 2014 (picha kumukumbu)
Patrick Karegeya, mkuu wa zamani wa idara ya ujasusi ya Rwanda, alizikwa Johannesburg Januari 19, 2014 (picha kumukumbu) © RFI/Alexandra Brangeon
Matangazo ya kibiashara

Ismael Gafaranga na Alex Sugira wanashukiwa na mahakama nchini Afrika Kusini kushiriki, mnamo mwaka 2014, katika mauaji ya mkuu wa zamani wa idara ya ujasusi nchini Rwanda, Patrick Karegeya, baada ya uhusiano na Rais Paul Kagame kuwa mbaya. Waranti hizo zinatolewa dhidi yao baada ya miaka mitano ya kesi hiyo mahakamani.

Mwezi Januari 1, 2014, Patrick Karegeya alipatikana amefariki dunia kwenye chumba chake cha hoteli mjini Johannesburg. Tangu mwanzo wa uchunguzi, mahakama nchini Afrika Kusini ilitambua haraka watuhumiwa wanne ambao wana uhusiano na serikali ya Paul Kagame.

Ili kuepusha mzozo wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili, ofisi ya mwendesha mashtaka ilikataa kuendelea na mashtaka dhidi ya watuhumiwa hao na hivyo kesi hiyo kusitishwa.

Kwa upande wa David Batenga, mpwa wa Patrick Karegeya, kutolewa kwa waranti hizi ni "ushindi wa kwanza".

"Tumesubiri muda mrefu sana. Tutaendelea kupambana ili wauaji warejeshwe kutoka katika nchi yetu. Hatutochoka na kwa bahati nzuri tunaishi katika nchi yenye sheria. Sio Rwanda. Kwa hivyo baadhi ya vizingiti vitachelewesha mahakama kufanya kazi yake, lakini tunajua kuwa haraka sana au baadaye, ukweli utajulikana na tutatendewa haki, " amesema David Batenga.

Gihanna Kennedy, mmoja wa mawakili wa familia, ana imani kuwa mahakama itatekeleza majukumu yake, lakini haamini kuwa washukiwa watarejeshwa nchini Afrika kusini.

"Kwa kweli tunajua kuwa serikali ya Rwanda haitokubali kuwasafirisha wanajeshi waje kwenda katika keshi katika nchi ya kigeni. Hata hivyo Afrika Kusini inaweza kuomba polisi ya kimataifa, Interpol, kuwakamata watu hao. Huu ni ujumbe muhimu, uliotumwa na mahakama huru ya nchi huru, " amesema mmoja wa mawakili wa familia ya Patrick Karegeya.

Karegeya alikuwa mkuu wa zamani wa ujasusi nchini Rwanda, na alipatikana amenyongwa katika hoteli moja mjini Johannesburg, Afrika Kusini.

Karegeya alikuwa mshirika wa karibu sana wa Kagame kabla ya kutofautiana naye.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.