Pata taarifa kuu
ALGERIA-MAANDAMANO-SIASA-UCHAGUZI

Bouteflika arejea Algeria, maandamano yaendelea

Rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika amerejea nchini Algeria siku ya Jumapili, ambapo waandamanaji wanaendelea na maandamano yao kupinga muhula wa tano wa rais huyo, ambaye yuko madarakani kwa miaka 20 sasa.

Waandamanaji wanaandamana dhidi ya muhula wa tano wa rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika, Algiers Machi 8, 2019.
Waandamanaji wanaandamana dhidi ya muhula wa tano wa rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika, Algiers Machi 8, 2019. © REUTERS/Zohra Bensemra
Matangazo ya kibiashara

Utawala wa bouteflika unaendelea kukumbwa na maandamano makubwa, tangu rais huyo kutangaza nia yake ya kuwania katika uchaguzi ujao kwa muhula wa tano. Bouteflika alikuwa hayupo nchini kwa muda wa wiki mbili baada ya kulazwa hospitalini nchini Switzerland kwa ajili ya "vipimo vya kitabibu".

Taarifa ya kurejea kwa rais Abdelaziz Bouteflika imethibitishwa na ofisi ya rais jijini Algiers.

Siku ya Jumapili, maelfu ya wanafunzi wa shule za sekondari kutoka nchi nzima waliandamana dhidi ya muhula wa tano wa Bouteflika, ambaye anatarajia kushiriki kinyang'anyiro cha urais katika uchaguzi uliopangwa kufanyika tarehe 18 Aprili. Waandamanaji waliitikia wito wa kuandamana uliotolewa kupitia mitandao ya kijamii.

Tangu Februari 22, Wananchi wa Algeria wameendelea kujitokeza mitaani huku wakimwomba rais Bouteflika, ambaye aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa (miaka 82) alipokuwa amelazwa hospitalini nchini Uswisi, kujiondoa katika kinyang'anyiro hicho cha urais.

Ugonjwa wa kiharusi alionao imemzuia Bouteflika kuhutubia moja kwa moja wananchi tangu mwaka 2013 na umemfanya kutoonekana mara kwa mara hadharani.

Jeshi "linaungana" na wananchi wa Algeria kwa "maadili sawa na kanuni", Mkuu wa majeshi ya Algeria na naibu waziri wa ulinzi Ahmed Gaïd Salah, amesema mbele ya wananfunzi wa vyuo kadhaa vya kijeshi siku ya Jumapili.

Hata hivyo maandamano makubwa yanatarajiwa leo Jumatatu katika miji mbalimbali ya nchi hiyo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.