Pata taarifa kuu
DRC

DRC: Polisi yawatuhumu waasi kwa mauaji ya maofisa wake zaidi ya 39

Polisi wa kitaifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia wanawatuhumu waasi kwa kuwaua maafisa wake 39 wakati wa machafuko yaliyoshuhudiwa kwenye mkoa wa Kasai.

Ramani ikionesha eneo la Tshikapa-Kananga, ambako mauaji ya halaiki yameripotiwa
Ramani ikionesha eneo la Tshikapa-Kananga, ambako mauaji ya halaiki yameripotiwa GOOGLE MAPS
Matangazo ya kibiashara

Maofisa hao waliuawa katika shambulio la kushtukiza siku ya Ijumaa na kuzikwa kwenye makaburi ya pamoja na wafuasi wa kiongozi wa zamani wa kijadi Kamwina Nsapu umbali wa kilometa 75 kaskazini mwa mji wa Tshikapa katikati ya jimbo la Kasai, amesema msemaji wa polisi.

Maofisa hao 39 waliuawa wakati wakisafiri kwa kutumia magari ya jeshi pamoja na mizigo mingine kama zana za jeshi la polisi, ambapo washambuliaji waliziteka, ameongeza kanali Pierre-Rombaut Mwanamputu.

Taarifa ya Polisi imesema kuwa, jeshi hilo linalaani mauaji hayo na limechukua hatua za dharura kuimarisha usalama kwenye eneo hilo na maeneo mengine ya nchi.

Eneo la Kasai ya Kati limeshuhudia machafuko toka katikati ya mwezi Agosti mwaka jana, baada ya vikosi vya Serikali kumuua Nsapu, mtawala wa kimila na kiongozi wa kundi la wapiganaji walioamua kushika silaha kupinga utawala wa rais Joseph Kabila.

Makabiliano kati ya wafuasi wa Nsapu na vikosi vya Serikali yalianzia kwenye mkoa wa Kasai ya kati, lakini toka wakati huo makabiliano hayo yameenea hadi kwenye maeneo jirani kama mkoa wa Kasai-Oriental na Lomami ambapo mpaka sasa watu 400 wamekufa.

Kundi la Kamwina Nsapu linatuhumiwa kwa matukio kadhaa ya mauaji na umoja wa Mataifa pamoja na kutumia watoto kama wanajeshi.

Hata hivyo vyombo vya usalama vya DRC pia vimekuwa vikipokea ukosolewaji kutoka kwenye umoja wa Mataifa kwa kutumia nguvu kubwa dhidi ya waandamanaji na wapiganaji wenye silaha.

Mwanzoni mwa mwezi huu, wanajeshi saba wa serikali ya DRC walikamatwa baada ya kusambaa kwa picha za video zilizowaonesha wanajeshi hao wakiwafyatulia risasi raia ambao hawakuwa na silaha kwenye jimbo la Kasai-Oriental.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.