Pata taarifa kuu
SIKU YA WANAWAKE DUNIANI 2017

Dunia itimize wajibu wake kwa wanawake na wasichana 50-50 ifikapo mwaka 2030

Dunia inabadilika huku mabadiliko haya yakiwa na athari kubwa kwa wanawake, lakini katika upande mwingine, maendeleo ya teknolojia na utandawazi yanatoa nafasi kwa wale ambao hawana uwezo wa kutumia, hata hivyo kunaendelea kushuhudiwa ongezeko kubwa la sekta za ajira zisizo rasmi, utofauti wa kipato na hali tete ya kibinadamu.

Mmoja wa wanawake nchini India akipuliza moto, hizi ni kazi ambazo UN inasema wanawake wanaishia kuzifanya
Mmoja wa wanawake nchini India akipuliza moto, hizi ni kazi ambazo UN inasema wanawake wanaishia kuzifanya REUTERS/Danish Siddiqui
Matangazo ya kibiashara

Kwa hali hii ya kurudi nyuma, ni asilimia 50 pekee ya wanawake wenye umri wa kufanya kazi ndio wanawakilishwa kidunia, ukilinganisha na asilimia 76 ya wanaume ambao wanafanya kazi na kulipwa mshahara.

Na cha kushangaza zaidi wanawake wengi wameajiriwa kwenye sekta zisizo rasmi za kiuchumi, wamekuwa ni watu wa kufanya kazi za nyumbani peke yake na kufanya kazi zenye ujira mdogo na zisizo na usalama kwao.

Kwa hivyo wanaharakati wa masuala ya wanawake wanasema kuwa, kufikia malengo ya usawa wa kijinsia dunia, ni kazi ya pamoja ya watu wote kwa maendeleo endelevu.

Ndio maana umoja wa Mataifa kupitia maadhimisho ya mwaka huu, unatoa wito kwa dunia kufanya kila namna kufikia usawa wa kijinsia kuelekea dunia ya asilimia 50 kwa 50 ifikapo mwaka 2030 na kwa kuhakikisha kuwa dunia ya kazi ni kwa wanawake wote pia.

Katika mkutano ujao wa taasisi ya wanawake wa umoja wa Mataifa utakaoanza Machi 13 hadi 24 jijini New York, utaelezea uwezeshaji wa wanawake kiuchumi katika kubadili mtazamo wa ajira ya dunia.

Wanawake nchini Marekani wakiandamana kutetea haki zao. Machi 5, 2017
Wanawake nchini Marekani wakiandamana kutetea haki zao. Machi 5, 2017 REUTERS/Lucy Nicholson

Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, anasema kuwa haki za wanawake ni haki za binadamu, lakini akaongeza kuwa nyakati hizi za mizozo dunia imekuwa haitabiriki na imeharibika, anasema haki za wanawake na wasichana zimepunguzwa, zimewekewa ukomo na kubadilishwa.

Guterres anasema kuwawezesha wanawake na wasichana ndio njia pekee ya kuwalinda na kulinda haki zao na kuhakikisha wanatimiza ndoto zao.

Wataalamu wanasema kupunguza ombwe la usawa wa kijinsia kwenye ajira kutaongeza dola za Marekani trilioni 12 kwenye pato ghafi la dunia kufikia mwaka 2025, na wanasema kwa kuongeza wigo wa wanawake kufanya kazi, kutawafanya wawe wawakilishi wazuri, wabunifu na kuendeleza maamuzi yao kwa jamii.

Suala la usawa wa kijinsia ni kiini na mzizi wa ajenda ya mwaka 2030 ya Maendeleo Endelevu na kwamba ajenda namba 5 ya Maendeleo Endelevu inasema wazi kabisa kuhusu usawa wa kijinsia na uwezeshaji kwa wanawake na wasichana wote na kwamba ni muhimu kufikia mafanikio haya katika ajenda zote 17 za Maendeleo Endelevu.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni "Wanawake katika kubadilisha ajira ya dunia: Sayari ya 50-50 ifikapo mwaka 2030".

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.