Pata taarifa kuu
DRC-KABILA

Nchi ya DRC yapata waziri mkuu mpya

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, amemtangaza waziri mkuu mpya kutoka muungano wa vyama vya upinzani vilivyoshiriki mazungumzo ya kitaifa yaliyomalizika hivi karibuni na kukubaliwa kuundwa kwa Serikali ya mpito kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2018.

Samy Badibanga (katikati) katika sherehe za ufunguzi wa mazungumo ya kitaifa mjini Kinshasa, tarehe 1 Septemba 2016.
Samy Badibanga (katikati) katika sherehe za ufunguzi wa mazungumo ya kitaifa mjini Kinshasa, tarehe 1 Septemba 2016. JUNIOR D.KANNAH / AFP
Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa tangazo kutoka ikulu ya Kinshasa lililosomwa kupitia televisheni ya taifa, Rais Kabila amemteua Samy Badibanga kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo.

Badibanga kabla ya uteuzi huu, alikuwa ni kiongozi wa vyama vya upinzani bungeni.

Uteuzi wa Badibanga umekuja baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa waziri mkuu Matata Ponyo, aliyeachia nafasi hiyo Jumatatu ya wiki hii, kufuatia makubaliano ambayo yamepingwa vikali na muungano wa upinzani wa Rassemblement ambao haukushiriki kwenye mazungumzo ya kitaifa.

Makubaliano haya ambayo awali yalifuatiwa na "mazungumzo ya kitaifa" yalilenga kutuliza mzozo wa kisiasa uliokuwa unafukuta nchini humo, sasa yakimaanisha kuwa, Rais Joseph Kabila ataendelea kusalia madarakani kwa angalau hadi mwishoni mwa mwaka 2017.

Rais Kabila, kwa mujibu wa katiba ya DRC, alitakiwa kuondoka ofisini Desemba 19 mwaka huu.

"Mkataba huu kwa sasa unawakilisha sehemu tu ya uelekeo ambao umekubaliwa na wananchi wa Kongo," alisema Rais Kabila wakati akihutubia bunge na wajumbe wa baraza la seneti juma hili.

Rais Kabila alidai kuwa yuko tayari kuheshimu katiba ya nchi na kwamba atahakikisha analinda makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni na kupambana na mtu yeyote ambaye atataka kuichukua nchi kwa nguvu, akiahidi uchaguzi utafanyika katika mazingira ya uhuru na haki.

Uteuzi wa Badibanga umeshangaza wengi kama ulivyomshangaza kiongozi wa chama cha UNC, VItal Kamerhe ambaye aliongoza muungano wa upinzani ulioshiriki kwenye mazungumzo hayo ya kitaifa, na alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kumrithi Matata Ponyo.

Badibanga aliingia kwenye siasa mwaka 1996, ambapo alijiunga na chama kikuu cha upinzani nchini DRC, cha UDPS kinachoongozwa na Etienne Tshisekedi, ambaye chama chake hakikushiriki mazungumzo ya kitaifa.

Badibanga alikuwa mshauri maalumu na mtu wa karibu wa Etienne Tshisekedi, kabla ya kufurushwa chamani, muda mfupi baada ya kukubali kushiriki kwenye mazungumzo ya kitaifa, ambayo chama chake hakikushiriki.

Uamuzi wa Badibanga kushiriki kwenye mazungumzo ya kitaifa bila kupata idhini ya kiongozi wake wa chama, ulileta mtafaruku mkubwa ndani ya chama chake, kiasi cha kutangaza kumfuta uanachama wake, lakini bado aliendelea kuwa kinara wa upinzani bungeni.

Baadhi ya wadadisi wa mambo wanaona kuwa uteuzi wake ni kama fadhila za Rais Kabila, baada ya kuona kinara huyo akiunga mkono mazungumzo ya kitaifa.

Wapo wanaodai kuwa, ukaidi wake wa kushiriki mazungumzo ya kitaifa, ulitokana na kesi zilizokuwa zikimkabili bungeni, na kwamba huenda uamuzi wake kushiriki kwenye mazungumzo, alikuwa akitaka msamaha wa Rais Kabila.

Nchi ya DRC imekuwa kwenye mivutano ya kisiasa toka kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2011 ambao Tshisekedi anadai aliibuka na ushindi, lakini hata hivyo rais Kabila alishinda kwa muhula wa pili.

Katiba iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2006, imeweka ukomo wa mihula miwili kwa Rais kukaa madarakani.

Machafuko makubwa zaidi yalishuhudiwa mwezi September mwaka huu, baada ya kuzuka kwa maandamano ya kuipinga Serikali, ambapo watu 53 waliuawa, hii ni kwa mujibu wa taarifa za Umoja wa Mataifa.

Rais Kabila alichukua madaraka mwaka 2001, siku 10 tu baada ya mauaji ya baba yake, ambaye alikuwa Rais wa nchi hiyo, Laurent Kabila.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.