Pata taarifa kuu
AFRIKA KUSINI

Taasisi ya mfuko wa Nelson Mandela yamtaka Rais Zuma kujiuzulu

Taasisi ya Nelson Mandela, iliyoundwa kwa lengo la kuhifadhi heshima ya muasisi wa taifa hilo na rais wa kwanza mweusi, Jumanne ya wiki hii imetoa taarifa ikimlaumu Rais Jacob Zuma kwa kusababisha sintofahamu nchini humo na kuteteresha uchumi wake.

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma.
Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma. REUTERS/Siphiwe Sibeko
Matangazo ya kibiashara

Toka alipoingia madarakani mwaka 2009, Rais Zuma tayari ameshakwepa kuondolewa madarakani mara kadhaa katika kura ya kutokuwa na imani nae bungeni, kutokana na kukabiliwa na kashfa za rushwa na matumizi mabaya ya ofisi.

Katika taarifa yake ya kipekee kuwahi kuitoa, taasisi ya mfuko wa Nelson Mandela, ambayo bodi yake inaundwa watu mashuhuri ambao ni wasomi, wanasiasa na waandishi wa habari, wametoa wito kwa chama tawala cha ANC, kufanya mabadiliko ya kiutawala.

"Tunatoa wito kwa chama tawala, kuchukua hatua zinazohitajika kuhakikisha taasisi za Serikali na katiba vinalindwa na kupewa mtu mwenye uwezo wa kuvilinda," imesema taarifa ya taasisi hiyo iliyopewa jina la "Muda wa kuiwajibisha Serikali dhalimu."

Hata hivyo kambi ya rais Jacob Zuma haijazungumza chochote kuhusiana na taarifa hii.

Rais Zuma amekuwa kwenye shinikizo kubwa hata kutoka ndani ya chama chake, ambapo baadhi ya wanachama wanamtaka aondoke madarakani, toka kushindwa vibaya kwa chama chao kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Hata hivyo licha ya shinikizo kutoka ndani ya chama, kamati kuu ya chama cha ANC imeendelea kumkingia kifua rais Zuma, ambapo imetangaza kuendelea kumuunga mkono.

Upinzani pamoja na mashirika ya kiraia, wamepanga kufanya maandamano makubwa jijini Pretoria siku ya Jumatano, Novemba 2, wakitaka, miongoni mwa mambo mengine, rais Zuma ajiuzulu nafaso yake.

Hata hivyo Rais Zuma hajaonesha dalili zozote za kuondoka madarakani hivi karibuni kabla ya kutamatika kwa muhula wake wa pili na wa mwisho mwaka 2019, licha ya kukabiliwa na tuhuma nzito za rushwa ambazo zimemsababishia pia hasara binafsi na kisiasa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.