Pata taarifa kuu
SIASA TANZANIA

Upinzani nchini Tanzania wakataa matokeo ya urais

Mgombea urais kupitia muungano wa vyama vya upinzani UKAWA nchini Tanzania Edward Lowasa amesema hatambui matokeo ya urais yanayoendelea kutangazwa na tume ya uchaguzi nchini humo kutokana na kile anachosema kura zake zimeibiwa.

Edward Lowasa mgombea wa upinzani
Edward Lowasa mgombea wa upinzani RFI Kiswahili
Matangazo ya kibiashara

Akizungumza na wanahabari hapa jijini Dar es salaam, Lowasa ameitaka tume kusitisha mara moja kutangaza matokeo hayo na kutaka kura kuhesabiwa upya kutumia njia za kawaida bila kutumia teknolojia.

Lowasa amewataka wafuasi wake kuendelea kuwa watulivu wakati huu viongozi wa upinzani wanapoendelea na vikao kuhusu hatua zaidi watakazozichukua.

“Nawaomba vijana wasalie katika hali ya utulivu na kuendelea kushikamana, tusilete vujo kwa sababu ukifanya hivyo tutawapa nafasi ya kuzungumza, tutawapa maelekezo zaidi,” alisema Lowasa.

Juma Haji Duni ambaye ni mgombea mwenza wa Lowasa amedai kuwa mgombea wa chama cha Mapinduzi John Magufuli ameongezewa kura ili kushinda uchaguzi huu.

Nacho Chama cha mapinduzi kimekanusha madai hayo ya upinzani na kusema serikali haitakubali taifa hilo kuingia kwenye machafuko.

“Ukawa wanaweza kulalamika usiku na mchana lakini hatuwezi kuruhusu nchi hii kuingia katika machafuko kwa sababu ya mtu mmoja,” alisema mmoja wa viongozi wa CCM jijini Dar es salaam Jumatano jioni.

Hali hii imezua sintofahamu kati ya wafuasi wa Ukawa na CCM huku tume ya uchaguzi ikiendelea kutangaza matokeo ya urais.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Jaji Mstaafu Damian Lubuva amesema matangazo ya kura za urais yanatarajiwa kumalizika siku ya Alhamisi na baadaye mshindi kutangazwa na kukabidhiwa cheti.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.