Pata taarifa kuu
BURUNDI-MAANDAMANO-USALAMA-SIASA

Wafuasi wa jenerali Nshimirimana waandamana Bujumbura

Nchini Burundi, wiki moja baada ya kifo cha luteni jenerali Adolphe Nshimirimana, wafuasi wa mkuu huyo wa zamani wa Idara ya Ujasusi wamekusanyika Jumapili Agosti 9 na kufanya maandamano wilayani Kamenge, Kaskazini mwa mji wa Bujumbura.

Waandamanaji walikua wamevaa nguo nyeusi, na waliandamana kuanzia mbele ya baa ya jeneraliAdolphe  Nshimirimana hadi mahali alipouawa, wilayani Kamenge, Kaskazini mwa jiji la Bujumbura.
Waandamanaji walikua wamevaa nguo nyeusi, na waliandamana kuanzia mbele ya baa ya jeneraliAdolphe Nshimirimana hadi mahali alipouawa, wilayani Kamenge, Kaskazini mwa jiji la Bujumbura. AFP PHOTO / GRIFF TAPPER
Matangazo ya kibiashara

Maandamano hayo ya kumkumbuka luteni jenerali Adolphe Nshimirimana yamefanyika katika ukimya na yamekua ya aina yake ya kipekee.

Haya ni maandamano ya kwanza kuruhusiwa tangu kuanza kwa machafuko nchini Burundi. Maandamano hayo yalipangwa kupitia mitandao ya kijamii, amesema Thomas, mmoja kati ya waandamanaji. " Tumekubaliana kuwa kila Jumapili kutakua kukifanyika maandamano ya kumkumbuka shujaa huyo hadi mazishi yake ", ameongeza Thomas. Waandamanaji walianza kukusanyika saa 12:30 asubuhi mbele ya baa ya luteni jenerali adolphe Nshimirimana, mjini Bujumbura, na maandamano yalianza saa 2:00 na huku wakielekea mahali alipouawa Adolphe Nshimirimana.

Wafuasi wa mkuu huyo wa zamani wa Idara ya Ujasusi walikuwa wamevaa nguo nyeusi huku wakibebelea mishumaa na mabango kama ishara ya kumkumbuka luteni jenerali Adolphe Nshimirimana. Kwa mujibu wa Thomas, walikuwa kati ya 1000 na 1500 katika maandamano hayo ya Jumapili asubuhi.

" Kulikuwa na maumivu mioyoni mwao, kwa sababu luteni jenerali Adolphe Nshimirimana alikuwa akipendwa na raia, hasa katika mji wa Bujumbura, katika maeneo yalio pembezoni mwa Kamenge ", amesema Thomas.

Itafahamika kwamba luteni jenerali Adolphe Nshimirimana tangu ujana wake aliishi wilayani Kamenge kabla ya kujiunga na kundi la zamani la waasi la CNDD-FDD, na katika wilaya hiyo ndipo aliuawa.

Uchunguzi " unaendelea vizuri "

Jumapili hii asubuhi, mwendesha mashtaka wa jamhuri amebaini kwamba uchunguzi kuhusu kifo cha mkuu wa zamani wa Idara ya Ujasusi unaendelea vizuri. Jumapili iliyopita, rais Nkurunziza alitoa muda wa wiki moja ili waliohusika na mauaji hayo wawe wamekamatwa.

 Katika taarifa iliyorushwa hewani kwenye mitandao ya kijamii, Ofisi ya mashtaka imesema inawatambua waliohusika na shambulio dhidi ya Adolphe Nshimirimana, lakini imesema kuwa baadhi yao walikamatwa, lakini wengine bado wanatafutwa. Utambulisho wao haukuwekwa wazi. Gari lilotumiwa na waliohusika katika shambulio hilo lilipatikana lilichomwa moto siku moja baada ya kifo cha luteni jenerali Adolphe Nshimirimana na sare walizovaa washambuliaji hao zilipatikana katika moja ya mifereji ya mjini Bujumbura.

Uchunguzi " unaendelea vizuri ", imesema taarifa hiyo, lakini Ofisi ya mashtaka imetoa wito kwa raia kusaidia kuwapata watu wote waliohusika na mauaji hayo.

Hayo yakijiri mwanaharakati maarufu wa haki za binadam, akiwa pia kiongozi wa shirika linalotetea haki za binadam nchini Burundi (APRODH), Pierre-Claver Mbonimpa amesafirishwa nchini Ubelgiji Jumapili Agosti 9 kwa ajili ya matibabu, baada ya wiki moja kulazwa katika hospitali ya Polyclinique Centrale de Bujumbura kufuatia majesraha aliyoyapata baada ya kupigwa risasi na mtu asiyejulikana Jumapili Agosti 2 jioni wakati alipokua akielekea nyumbani kwake katika kata ya Carama, wilayani Kinama, kaskazini mwa jiji la Bujumbura.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.