Pata taarifa kuu
DRC-MONUSCO-ADF-USALAMA

Monusco yatazama jinsi ya kushirikiana na FARDC

Jeshi la Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Monusco linasema kuna haja kubwa ya kushirikiana na jeshi la nchi hiyo kuwalinda raia baada ya kutokea kwa mauaji ya raia katika wilaya ya Beni Ijumaa iliyopita.

Wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakiwa pamoja na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, Monusco katika wilaya ya Beni, Desemba 3 mwaka 2014.
Wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakiwa pamoja na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, Monusco katika wilaya ya Beni, Desemba 3 mwaka 2014. MONUSCO/Abel Kavanagh
Matangazo ya kibiashara

Mkuu wa Monusco Martin Kobler, katika ujumbe alioandika katika ukarasa wake wa Twitter amesema, ushirikiano huu unahitajika ili kusitisha mauaji hayo ambayo tangu mwezi Oktoba mwaka jana raia takribani 300 wameuawa na waasi wa ADF NALU.

Ijumaa iliyopita watu saba waliuawa katika eneo la Matembo Kilomita 10 kutoka mjini Beni baada ya kuvamiwa na watu waliokuwa wamejihami.

Monusco ilitangaza kusitisha kushirikiana na jeshi la Serikali ya DRC baada ya serikali kukataa kuwachukulia hatua majenerali wawili katika wa jeshi la Congo, ambao Monusco inasema wametekeleza visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu Mashariki mwa nchi hiyo.

Hayo yakijiri waziri wa sheria wa serikali ya DRC, Alexis Tambwe Mwamba, amesema serikali yake haitavumilia kuendelea kuona waasi wa Uganda wa ADF wanaendelea kuuwa wananchi wake wilayani Beni mkoani Kivu Kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Waziri Tambwe aliyasema hayo wakati wa ziara yake Jumapili mwishoni mwa juma hili lililopita mjini Goma, baada ya kukutana na gavana wa mkoa huo wa kivu kaskazi ni Julien Paluku

Kumeshuhudia mauaji mengine mapya ya watu saba usiku wa kuamkia Jumamosi mwishoni mwa juma hili lililopita katika mji wa Matembo eneo la Mulekera kilomita chache kutoka mjini Beni. Maiti za watu hao ziligunduliwa zikiwa na majeraha ya kushambuliwa kwa mapanga, shoka na visu.

Waasi wa ADF ambao walianzisha uasi katika nchi jirani ya Uganda dhidi ya raisi Museveni wanatuhumiwa kutekeleza mfululizo wa mashambulizi jirani na mji wa Beni na kusababisha vifo vya takribani watu mia 3 tangu mwezi Octoba mwaka jana.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.