Muda uliotolewa kwa waasi wa FDLR wamalizika
Januari 2 ni siku ya mwisho kwa muda uliyotolewa kwa waasi wa Kihutu wa Rwanda wa FDLR kuwa wawe wameshajisalimisha na kuweka silaha chini.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Jumuiya za kikanda, ICGLR na SADC, zikiungwa mkono na jumuiya ya kimataifa yalikuwa yametoa siku ya leo kuwa siku ya mwisho kwa waasi wa kundi la FDLR kuwa wameshajisalimisha kwa hiari yao na kukubali kupelekwa katika kambi iliyojengwa kwa minajili ya kurejeshwa katika maisha ya kiraia.
Kwa wale wote ambao watakua bado kujiunga na wengine katika mpango huo watalazimika kupokonywa silaha zao kwa nguvu katika operesheni ya pamoja ya kijeshi itakayoendeshwa na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na kikosi cha wanajeshi wa Umoja wa Mataifa nchini Congo Monusco.
Wapiganaji 400 kwa jumla ya wapiganaji walio kati ya 1500 na 3000, kulingana na takwimu, ndio wameshajiunga na mpango huo, katika kambi iliyojengwa na Monusco.
Kwa upande wake kundi la waasi wa Kihutu wa Rwanda la FDLR limebaini kwamba operesheni hizo hazina maana yoyote na zina lengo tu ya kumwaga damu ya raia wasio na hatia, ikiwa ni pamoja na wapiganaji waliopokonywa silaha pamoja na raia wa kawaida wanaishi pamoja nao.
" Jumuiya ya kimataifa ina kosa kwa sababu imekataa kutekeleza ombi letu kwa kuishinikiza serikali ya Rwanda kufungua nafasi kwa wanasiasa na kuhakikisha haki na uhuru wa wananchi wake", msemaji wa FDLR, La Forge Bazeye Fils ameiambia RFI.