Pata taarifa kuu

Ceni yakubali kuwepo na udanganyifu

Tume huru ya uchaguzi nchini Burundi imekubali kwamba kulikua na udanganyifu katika zoezi la kuandika wapiga kura.

Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi Burundi (CENI), Pierre Claver Ndayicariye.
Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi Burundi (CENI), Pierre Claver Ndayicariye. DR.
Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa tume hiyo, Prosper Ntahogwamiye, amesema vitambulisho vya uraia vilitolewa kiholela, huku kukionekana watu wakijiandikisha kwa kutumia vitambulisho bandia. Lakini msemaji huyo wa tume huru ya uchaguzi amebaini kwamba Wizara ya mambo ya ndani ndio inahusika na utoaji wa vitambulisho hivyo, wala si Céni.

Céni kupitia msemaji wake huyo imebaini kwamba Wizara ya mambo ya ndani ndio inapaswa kunyooshewa kidole cha lawama kutokana na zoezi hilo la utoaji wa vitambulisho vya uraia.

Kauli hiyo inakuja baada ya vyama 18 vya upinzani kuiomba tume huru ya uchaguzi (Céni) kujiuzulu haraka iwezekanavyo bila masharti.

Vyama hivyo 18 vya upinzani vinaitumu Céni kutowajibika kwa kazi yake, na kwamba ilikua ikifumbia macho dosari hizo ziliyojitokeza katika zoezi la kuandika wapiga kura.

Itafahamika kwamba tangu mwanzoni mwa zoezi la kuandika wapiga kura, upinzani na vyama vya kiraia vililalamikia dosari hizo na kuomba tume huru ya uchaguzi kusitisha zoezi hilo bila mafanikio.

Céni ilinyooshewa cha lawama kwamba imekua ikiegemea upande wa chama madarakani Cndd-fdd, kwa kufumbia macho dosari ambazo zilikua zikijitokeza katika zoezi la kuandika wapiga kura.

Hivi karibuni Wizara ya mambo ya ndani ilikubali pia kuwa kulikua na udanganyifu katika zoezi la utoaji wa vitambulisho vya uraia, lakini Waziri wa mambo ya ndani, Edouard Nduwimana, alibaini kwamba mchakato wa uchaguzi haumuhusu, bali unaihusu tume huru ya uchaguzi, kwani zoezi la utoaji vitambulisho vya uraia linaendana sambamba na mchakato wa uchaguzi ambao ni katika majukumu ya tume huru ya uchaguzi.

Hivi karibuni mkuu wa polisi, Andrès Ndayambaje, alivionya vyama vya kiraia pamoja na upinzani kutoendelea kuwakamata watu ambao wamekua wakijihusisha na utoaji wa vitambulisho bandia, akibaini kwamba si kazi yao, bali ni kazi ya polisi.

Andrès Ndayambaji aliwalaumu baadhi ya wanaharakati wa haki za binadamu pamoja na upinzani kwamba wamekua wakijihusisha na kazi ya polisi.

Hata hivyo Shirika linalotetea haki za binadamu na za wafungwa (Aprodh), limekua likiwakamata watu ambao wamekua wakijihusisha na utoaji wa vitambulisho bandia na kuwakabidhi kwa vyombo husika. Hivi karibuni kiongozi wa shirika hilo, Pierre-Claver Mbonimpa, alikamata vitambulisho bandia zaidi ya 200 katika wilaya ya Kamenge na Musaga jijini Bujumbura.

Katika mkutano na vyombo vya habari, Pierre-Claver Mbonimpa alionyesha vitambulisho hivyo alivyokamata katika wilaya hizo, akitolea wito Céni tume huru ya uchaguzi kusitisha zoezi la kuandika wapiga kura.

 Upinzani umetishia kutolea wito wafuasi wao ili waingiye barabarani iwapo hawatosikilizwa na madai yao yakapatiwa ufumbuzi.

Wizara ya mambo ya ndani na tume huru ya uchaguzi vimewataka wanasiasa wote kukutana kwa mazungumzo Jumatatu Desemba 22 ili kutafutia ufumbuzi tatizo hilo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.