Pata taarifa kuu
MISRI

Shinikizo zaendelea kutolewa kwa Misri kuwaachilia huru wanahabari wa Al-Jazeera

Shinikizo zinaendelea kutolewa kwa serikali ya Misri kuwaachilia huru wanahabari watatu wa kituo cha Al-Jazeera waliohukumiwa jela miaka 7 kwa kosa la kushirikiana na kundi la Muslim Brotherhood lililoharamishwa na kutoa habari za uongo.

Wanahabari wa Al-Jazeera
Wanahabari wa Al-Jazeera REUTERS/Asmaa Waguih
Matangazo ya kibiashara

Wanahabari hao ni pamoja na Peter Greste raia wa Australia, Mohamed Fadel Fahmy na Baher Mohamed wameendelea kukanusha tuhma dhidi yao.

Waandishi wengine 11 wa Al-Jazeera ambao hawakuwa Mahakamani nao walihukumiwa jela miaka 10, wakiwemo Wanahabari wawili kutoka Uholanzi na Uingereza.

Australia imesema inawasiliana moja kwa moja na serikali ya Misri kuiomba kuwaachilia huru Wanahabari hao ambao inasema wao walikwenda tu kufanya kazi yao na hawana ushirikiano na kundi la Muslim Brotherhood.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry amelaani hukumu hiyo na kuongeza kuwa Marekani pia inazungumza na rais Abdel Fattah al-Sisi kumwomba kuwaachilia huru wanahabari hao.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Josh Earnest amesema, serikali yake inaitaka serikali ya Misri kuwaachilia huru wanahabari hao bila ya masharti yoyote na pia kutoa msamaha kwa wafungwa wote wa kisiasa nchini humo.

Waziri wa Mambo ya nje wa Australia Julie Bishop naye amesema kesi hizo zilichochewa kisiasa na serikali ya Misri imeshindwa kuthibitisha kuwa wanahabari hao walitekeza makosa hayo.

Familia za wanahabari hao wamesema kuwa watakata rufaa kuhakikisha kuwa ndugu zao wanaachiliwa huru na kurudi nyumbani.

Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa Navi Pillay naye pia ameshutumu hukumu hiyo ambayo amesema ni ukiukwaji wa haki za binadamu na uhuru wa waandishi wa Habari duniani.

Mataifa kadhaa barani Ulaya yamesema yatawahoji Mabalozi wa Misri katika nchi zao kuhusu hukumu iliyotolewa dhidi ya wanahabari hao.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.