Pata taarifa kuu
KENYA-ICC

Majaji wa ICC waahirisha kesi ya rais Kenyatta hadi mwakani

Mahakama ya Kimataifa ya Uhlaifu wa kivita ya ICC imeahirisha kesi inayomkabili rais wa Kenya Uhuru Kenyatta hadi mwezi Februari mwakani.

Matangazo ya kibiashara

Kuahirishwa huko kunamaanisha kuwa kesi dhidi ya Kenyatta ambayo ilitarajiwa kuanza tarehe 12 mwezi huu wa Novemba sasa itaanza tarehe 5 mwezi wa Februari   baada ya Mawakili wake kuomba iahirishwe ili washughulikie maswala tata kuhusu ushahidi.

Majaji wa Mahakama hiyo wameeleza kuwa uamuzi huo pia umefikiwa baada ya kiongozi wa Mashtaka Fatou Bensouda kuridhia ombi la Kenyatta ili nao wapate muda wa kuandaa mashahidi wao baada ya Mahakama kuwaruhusu kuwaongeza mashahidi wawili zaidi.

Mawakili wa Kenyatta waliwaomba Majaji wa Mahakama hiyo kuahirisha kesi hiyo kwa miezi mitatu zaidi kushughulikia madai ya upande wa Mashtaka kuwa walikuwa wanaingilia ushahidi wa utetezi kwa kuwahonga mashahidi kubadilisha ushahidi wao dhidi ya rais Kenyatta.

Uamuzi huu pia unakuja wakati wajumbe wa Umoja wa Afrika wakikutana na wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakiliomba kuagiza Mahakama ya ICC kuahirisha kesi dhidi ya viongozi kwa Kenya kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Umoja wa Afrika unasema kuwa kuahirishwa kwa kesi hiyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa viongozi wa Kenya kushughulikia changamoto za kiusalama zinazoikabili  Kenya baada ya kundi la kigaidi la Al Shabab kulishambulia jengo la kibiashara la Westgate jijini Nairobi mwezi Septemba na kusababisha watu 67 kupoteza maisha.

Hata hivyo, juhudi zozote za kuahirisha kesi dhidi ya Kenyatta zinapingwa na upande wa Mashtaka ambao pia unasema kuwa kesi hiyo isiahirishwe tena kwa kile inachosema itahitilafiana na ushahidi wake.

Mwezi uliopita, Majaji wa Mahakama hiyo walimruhusu rais Kenyatta kutohudhuria vikao vyote vya kesi yake ambavyo kiongozi wa Mashtaka anataka ubadilishwe baada ya ombi kama hilo dhidi ya Ruto kukataliwa.

Rais Uhuru Kenyatta, Naibu wake William Ruto na Mwandishi wa Habari Joshua Arap Sang wanashtumiwa na Mahakama hiyo kwa kupanga, kufadhili na kuchochea machafuko ya baada ya Uchaguzi Mkuu nchini Kenya mwaka 2007 na kusababisha zaidi ya watu 1,000 kupoteza maisha na maelfu kukimbia makwao

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.