Pata taarifa kuu
KENYA- SOMALIA

Jeshi la Kenya lashambulia ngome ya Al Shabab nchini Somalia

Ndege za kivita za jeshi la Kenya zimetekeleza shambulizi la angaa katika kambi ya kundi la kigaidi la Al Shabab katika jimbo la Dinsoor Kilomita 300 kutoka mjini Mogadishu nchini Somalia.

Matangazo ya kibiashara

Jeshi la Kenya linasema kuwa kambi hiyo imekuwa ikitumiwa kuwapa mafunzo magaidi walioshambulia jengo la kibiashara la Westgate jijini Nairobi mwezi Septemba na kusababisha vifo vya watu 67.

Ripoti zinasema kuwa magari na hifadhi ya silaha za kundi hilo zimeharibiwa na wanajeshi wa Kenya katika oparesheni hiyo ya hivi punde iliyofanywa siku ya Alhamisi.

Wakati wa uvamizi huo, kambi hiyo ilikuwa na wanamgambo wa Al Shabab 300 waliokuwa wanapewa mafunzo na jeshi la Kenya linasema limewaua na kuwajeruhi wengi wao.

Kundi la Al Shabab halijazungumzia oparesheni hiyo ambayo jeshi la Kenya linasisitiza kuwa litaendelea kuzitekeleza kwa usaidizi na jeshi la Umoja wa Afrika ili kumaliza ngome za kundi hilo.

Siku ya Jumatatu juma hili, ndege zisizokuwa na rubani za Marekani zilishambulia viongozi wa juu wa kundi hilo na kufanikiwa kuwaua wawili Kusini mwa nchi hiyo.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kupitisha azimio la kuongezwa kwa wanajeshi zaidi wa Umoja wa Afrika AMISOM  ili idadi yao ifikie 22,000 kutoka ile ya sasa ambayo ni 17,000.

Kundi la kigaidi la Al Shabab ambalo sasa linashirikiana kwa karibu na lile la Al aeda linasalia kuwa hatari kwa usalama wa kanda ya Afrika Mashariki.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.