Pata taarifa kuu
SOMALIA-UN

UN kupitisha azimio la kuidhinisha majeshi zaidi kutumwa nchini Somalia

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kupitisha azimio la kuidhinisha kupelekwa kwa wanajeshi zaidi ya 4,000 nchini Somalia kusaidiana na wale wa Umoja wa Afrika wanaopambana na kundi la kigaidi la Al Shabab.

Matangazo ya kibiashara

Ikiwa azimio hilo litaidhinishwa kutakuwa na wanajeshi wa Umoja wa Afrika 22,000 nchini Somalia kupambana na kundi hilo la kigaidi baada ya kuonesha kuwa bado ni tishio kutokana na shambulizi la jengo la kibiashara la Westagte jijini Nairobi mwezi uliopita na kusababisha zaidi ya watu 67 kupoteza maisha.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson amewaambia wajumbe wa Baraza la Usalama kuwa jeshi la Umoja wa Afrika limekuwa likikumbana na wakati mgumu wa kusonga mbele kwa sababu ya idadi ndogo ya wanajeshi wa Umoja wa Afrika.

Umoja wa Afrika ulituma jeshi lake mara ya kwanza mwaka 2007 chini ya mwavuli wa AMISOM nchini SomaliaΒ  kupambana na wanamgambo hao na wamekuwa wakifadhiliwa na Umoja wa Ulaya na Mashirika mengine ya Kimataifa.

Jeshi la Umoja wa Afrika linalopambana na Al Shabab nchini Somalia linaundwa na mataifa yaΒ  Kenya, Uganda, Burundi na Djibouti mataifa ambayo yameendelea kupata vitisho kutoka kwa Al Shabab wanaotishia kushambulia nchi zao kwa kile wanachosema wamewavamia.

Mapema juma hili viongozi wawili wa juu wa kundi la kigaidi la Al Shabab nchini Somalia wameuawa baada ya msafara wao kushambuliwa na ndege ya Marekani isiyokuwa na rubani katika mji wa Jilib.

Mapema mwezi huu, wanajeshi wa Marekani walijaribu bila mafanikio Pwani ya Somalia kujaribu kumuua kiongozi wa juu wa Al-Shabab na kupata upinzani mkali kutoka kwa wanamgambo hao.

Marekani imeendelea kutumia ndege zisizokuwa na rubani kuwalenga wanamgambo wa Al- Shabab na mwaka 2008 ilifanikiwa kumuua Kamanda wa wanamgambo hao Aden Hashi Ayro.

Marekani imeweka kambi kubwa ya kijeshi katika nchi ya Djibouti karibu na Somalia kupambana na Al-Shabab.
Β 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.