Pata taarifa kuu
MISRI-MAREKANI

Misri yakosoa hatua ya Marekani kuisitishia ufadhili wa kijeshi

Misri imekosoa hatua ya Marekani kusitisha ufadhili wake wa kifedha wa Dola Bilioni 1 nukta 3 kulisaidia jeshi lake kununua vifaa vya kijeshi na kufanya mazoezi ya pamoja kati ya nchi hizo mbili.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa serikali ya mpito nchini Misri amesema kuwa hatua hiyo ya Marekani sio sahihi, na Cairo haitajisalimisha kwa Marekani kutokana na shinikizo zao.

Waziri wa Mambo nje wa Marekani John Kerry amesema kuwa kilichofanyika sio kuharibu uhusiano kati ya Marekani na Misri na urafiki kati ya mataifa hayo unasalia pale pale na lengo lao ni kuisaidia serikali hiyo ya mpito baada ya kupitia kipindi kigumu.

Washington DC imesema ilichukua  uamuzi huo umechukuliwa kutokana na kudorora kwa hali ya kisiasa nchini Misri na msaada huo utarejelewa  tu baada ya utulivu wa kisiasa kushuhudiwa tena nchini humo.

Marekani ilikuwa imeonya kuichukulia Misri hatua hii baada ya jeshi kuanza kuwasaka wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani Mohammed Mosri na kusababisha vifo vya mamia ya wafuasi wa chama cha Muslim Brotherhood mwezi wa Agosti.

Msemaji wa Wizara hiyo Jen Psaki amesema serikali ya mpito nchini Misri imejulishwa kuhusu hatua hiyo na ushirikiano huo utarudi kama kawaida baada ya kufanyika kwa Uchaguzi utakaokuwa huru na haki nchini humo.

Mbali na msaada huo wa mara ka mara wa kijeshi, Marekani ilikuwa imepanga kutoa msaada wa Dola Milioni 260 na kutoa mkopo wa Dola 300 kwa serikali ya Misri msaada ambao pia umesitishwa.

Mwezi uliopita, rais Barrack Obama akizungumza katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa alikashifu namna Mosri alivyoondolewa madarakani na jeshi na kusisitiza uwepo wa suluhu la kisiasa nchini humo kwa kuwashirikisha washikadau wote.

Wakati hayo yakijiri, Mahakama nchini Misri siku ya Jumatano ilitenga tarehe 4 mwezi wa Novemba kuanza kusikilizwa kwa kesi ya uchochezi na mauaji inayomkabili rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Morsi.

Morsi atafika kizimbani akiandamana na washtakiwa wengine 14 wanaotuhumiwa kuchochea mauaji hayo wakati wa maandamani mwezi Desemba mwaka uliopita, miezi saba kabla ya  uongozi wake haujapinduliwa na jeshi.

Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa kushtakiwa kwa Morsi huenda kukasababisha maandamano zaidi nchini humo kipindi hiki hali ya wasiwasi ikiendelea kutanda baada ya watu 57 kuuliwa Jumapili iliyopita wakati wa makabiliano na polisi jijini Cairo.

Upande wa Mashtaka unamtuhumu Morsi kuchochea maaandamano na mauji ya raia wasiokuwa na hatia mwaka uliopita kwa kutumia mamlaka yake vibaya kama kiongozi wa taifa hilo.

Wapinzani wa Morsi walianza kupiga kambi nje ya Ikulu jijini Cairo kumtuhumu kushindwa kutekeleza mabadiliko muhimu aliyowaahidi alipoingia madarakani baada ya mapinduzi dhidi ya rais wa zamani Hosni Mubarak.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.