Pata taarifa kuu
MISRI

Hofu yatanda Misri baada ya kuuliwa kwa wanajeshi na askari

Hofu imeendelea kutanda nchini Misri baada ya watu wenye silaha kushambulia Makao Makuu ya Polisi Kusini mwa eneo la Sinai na kusababisha vifo vya askari watatu kabla ya kuwashambulia wanajeshi katika Jiji la Ismailiya na kuwaua sita.

Matangazo ya kibiashara

Wizara ya Mambo ya Ndani nchini humo imethibitisha kushambuliwa kwa askari hao na wanajeshi na kusema watu waliotekeleza shambulizi hilo baya ni wanamgambo wenye lengo la kudhoofisha hali ya usalama katika nchi hiyo.

Mashambulizi haya yaliyotekelezwa na wanamgambo waliokuwa wamejihami vilivyo na silaha hatari yamekuja baada ya wananchi wa Misri kufanya kumbukizi ya miaka arobaini tangu kumalizika kwa vita kati yao na Israel.

Maadhimisho hayo yalitumiwa na wafuasi wa Chama Cha Muslim Brotherhood anachotokea Rais aliyeondolewa madarakani na Jeshi Mohamed Morsi kama sehemu yao ya kupaza sauti na kushinikiza Kiongozi wao arudishwe madarakani.

Mwishoni mwa juma lililopita, zaidi ya watu 50 waliuawa nchini humo baada ya makabiliano kuzuka kati ya wafuasi wa Morsi na polisi.

Wafuasi wa Mosri 200 kutoka chama cha Muslim Brotherhood wamekamatwa, baada ya kuendelea kusisitiza kuwa ni sharti kiongozi wao Morsi aliyeondolewa uongozini na jeshi arejeshwa madarakani.

Waziri Mkuu Hazem Beblawi ametoa wito kwa wananchi wa taifa hilo kusalia kuwa watulivu kipindi hiki taifa hilo likijaribu kujijenga upya baada ya kipindi kirefu cha machafuko.

Mamia ya wafuasi wa Morsi wamepoteza maisha tangu mwezi Julai mwaka huu wakati kiongozi wao alipoondolewa madarakani kutokana na maandamano makubwa ya wananchi waliosema ameshindwa kuleta mabadiliko.

Mosri kwa sasa anazuiliwa na jeshi ambalo liliteua serikali ya mpito kuongoza nchi hiyo huku uchaguzi mpya ukisubiriwa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.