Pata taarifa kuu
MISRI

Watu zaidi ya 50 wauawa nchini Misri katika makabiliano na polisi

Zaidi ya watu 50 wameuawa nchini Misri baada ya makabiliano kuzuka kati ya wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani Mohammed Morsi na polisi.

Matangazo ya kibiashara

Makabiliano hayo yalizuka mwishoni mwa juma lililopita wakati wa kuadhimisha miaka 40 kukumbuka vita vya mataifa ya kiarabu dhidi ya Israel katika maadhimisho hayo yaliyofanyika jijini Cairo.

Wafuasi wa Mosri 200 kutoka chama cha Muslim Brotherhood wamekamatwa, baada ya kuendelea kusisitiza kuwa ni sharti kiongozi wao Morsi aliyeondolewa uongozini na jeshi arejeshwa madarakani.

Maelfu ya raia wa Misri walikuwa wamekusanyika katika viwanja vya Tahrir na kuadhimisha miaka 40 ya mapambano hayo wakati machafuko yalipoanza, huku baadhi ya wafuasi wa serikali ya mpito wakionekana kubeba mabango yalionesha kuunga mkono serikali hiyo suala lililowakasirisha wafuasi wa Morsi.

Wizara ya mambo ya ndani imeonya kuwa itamchukulia hatua yeyote atakayebainika kuchochea vurugu nchini humo.

Waziri Mkuu Hazem Beblawi ametoa wito kwa wananchi wa taifa hilo kusalia kuwa watulivu kipindi hiki taifa hilo likijaribu kujijenga upya baada ya kipindi kirefu cha machafuko.

Mamia ya wafuasi wa Morsi wamepoteza maisha tangu mwezi Julai mwaka huu wakati kiongozi wao alipoondolewa madarakani kutokana na maandamano makubwa ya wananchi waliosema ameshindwa kuleta mabadiliko.

Mosri kwa sasa anazuiliwa na jeshi ambalo liliteua serikali ya mpito kuongoza nchi hiyo huku uchaguzi mpya ukisubiriwa.

Wiki iliyopita Mkuu wa sera ya nje wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton alikuwa jijini Cairo na kuwashawishi viongozi wa serikali ya mpito kushirikiana na washikadau wote ili kupatikana kwa suluhu la kisiasa nchini humo.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.