Pata taarifa kuu
KENYA

Mahakama ya Juu nchini Kenya yatoa maelezo kamili kuhusu kesi ya urais

Mahakama ya Juu nchini Kenya hatimaye imetoa maelezo ya kina kuhusu uamuzi wao wa wiki mbili zilizopita kuthibitisha ushindi wa rais Uhuru Kenyatta kama mshindi halali wa Uchaguzi Mkuu uliopita.

Matangazo ya kibiashara

Jaji Mkuu wa Kenya Willy Mutunga ambaye pia ni rais wa Mahakama hiyo amesema uamuzi wa Mahakama hiyo utatolewa kwa umma kupitia vijitabu ili wajisomee wenyewe na kufahamu sababu za uamuzi wao.

Mutunga pia ameiagiza tume ya kitaifa ya kutoa mafunzo kwa wafanyikazi wa idara ya Mahakama kutoa maelezo ya kina kwa umma kupitia mikutano mbalimbali.

Uamuzi huo pia utatolewa kwa vyombo vya habari ili kuwafikia wakenya wengi nchini humo.

Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga aliwasilisha kesi katika Mahakama hiyo ya juu kupinga matokeo ya tume ya Uchaguzi nchini humo kumtangaza Uhuru Kenyatta kama mshindi kwa madai kuwa kulikuwa na wizi wa kura.

Uamuzi wa Mahakama hiyo mwisho wa mwezi wa tatu uliotolewa na Majaji wa Mahakama hiyo ya juu na kuamua kuwa Uhuru Kenyatta alishinda uchaguzi huo kwa njia ya huru na haki na alitangazwa kwa misingi ya Kikatiba nchini humo.

Licha ya Waziri Mkuu wa zamani Odinga kukubali uamuzi wa Mahakama hiyo, alisema kuwa hakukubaliana na sababu zilizotolewa na Majaji wa Mahakama hiyo.

Odinga alisema kuwa alionewa na Majaji hao ambao walitupa ushahidi wake na kusema alisulubiwa na Mahakama hiyo.

Uhuru Kenyatta aliapishwa kuwa rais wa nne wa Kenya wiki iliyopita na Jumanne hii analifungua bunge la kitaifa na Senate jijini Nairobi.

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.