Pata taarifa kuu
TUNISIA

Vurugu zazuka nchini Tunisia baada ya kutangazwa matokeo ya mwisho ya Ubunge

Ghasia zimezuka nchini Tunisia katika Mji wa Sidi Bouzid na kuwalazimu polisi kutumia mabomu ya machozi kuwasambaratisha mamia ya wananchi ambao walikuwa wanashinikiza kufutwa kwa baadhi ya matokeo ya ubunge ambayo yametangazwa na kuonesha Chama Cha Kiislam chenye uungwaji mkono cha Ennahda kikishinda.

REUTERS/Zohra Bensemra
Matangazo ya kibiashara

Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tunisia ilitangaza matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa Ubunge wa kwanza wa kidemokrasia kufanyika katika miongo kadhaa kisha kufuatiwa na maandamano yaliyozingirwa na ghasia yakitaka kufutwa kwa matokeo ya chama kimoja.

Mji wa Sidi Bouzid ndiyo kitovu cha ghasia ambazo zilizuka nchini Tunisia mapema mwaka huu na kusababaisha kuangushwa kwa Utawala wa Rais Zine El Abidine Ben Ali kutokana na wananchi kudai wamekuwa wakikabiliwa na hali ngumu ya maisha.

Matokeo ya mwisho ya Uchaguzi huo wa Ubunge nchini Tunisia yanaonesha kuwa Chama Cha Kiislam cha Ennahda kimeshinda uchaguzi huo uliofanyika siku ya jumapili kwa asilimia arobaini na moja.

Kiongozi wa Chama Cha Ennahda Rached Ghannouchi amesema serikali mpya itaendelea kufanya mapinduzi yanayoitajika kwa kuwa Tunisia ni ya kila mwananchi na anastahili kunufaika ya rasilimali za taifa hilo.

Chama Cha Ennahda kimefanikiwa kupata viti tisini vya ubunge kati ya mia mbili na kumi na saba na tayari Chama hicho kilitangaza kuhakikisha serikali mpya inaundwa haraka iwezekanavyo.

Tayari Chama Cha Ennahda kinatarajiwa kumpendekeza Katibu Mkuu wake Hamadi Jebali kuwa Waziri Mkuu wakati huu ambapo kinaendelea na mazungumzo ya kuunda serikali ya Umoja na Vyama vya CPR na Ettakatol.

Tunisia imefanya uchaguzi wake wa kwanza wa kidemokrasia ikiwa ni miezi tisa baada ya kuangushwa kwa Utawala wa Rais Ben Ali ambaye alikaa madarakani kwa kipindi cha miaka ishirini na mitatu.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.