Pata taarifa kuu
EQUATORIAL GUINEA-LIBYA

Viongozi wa Umoja wa Afrika AU washindwa kuafikiana juu ya mgogoro wa Libya

Mkutano wa Viongozi wa Umoja wa Afrika AU ambao unafanyika Jijini Malabo nchini Equatorial Guinea kwa siku mbili umeshuhudia siku ya kwanza ukitawaliwa na mjadala mkali juu ya hatima ya mgogoro unaoendelea nchini Libya bila ya kupatikana kwa suluhu ya nini kifanyike. 

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma akiongoza moja ya vikao vya kutafuta suluhu nchini Libya
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma akiongoza moja ya vikao vya kutafuta suluhu nchini Libya AFP / ALEXANDER JOE
Matangazo ya kibiashara

Viongozi hao wametumia siku ya kwanza ya Mkutano huo kwa kuangalia namna ya kufanikisha kumaliza mgogoro uliozuka nchini Libya kati ya Majeshi ya Kanali Muammar Gaddafi dhidi ya Waasi.

Mjadala mkali umetawala kikao hicho ambapo hakuna muafaka ambao ulifikiwa katika siku ya kwanza kutokana na Viongozi hao kugawanyika kimsimamo juu ya nini iwe suluhu ya kudumu ya mtafaruku huo.

Mkutano huo ambao unahudhuriwa na wajumbe kutoka Utawala wa Kanali Gaddafi na Waasi unajikita katika kuangalia ni namna gani utafanikisha kupatikana kwa muafaka katika nchi hiyo kwa sasa.

Viongozi hao wamesigana juu ya mafikiano yao hatua ambayo ilichangia kuyapeleka mbele mazungumzo hayo hadi mapema leo asubuhi ambapo wanatarajia kuibuka na msimamo wa pamoja.

Mapema Mwakilishi wa Waasi kwenye Mkutano huo wa AU Mansour Al Nasr amenukuliwa akisema wao watakuwa tayari kuweka silaha chini iwapo Kanali Gaddafi ataondoka madarakani kinyume na hapo watapigana hadi wafanikishe nia yao.

Naye Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika AU Jean Ping alipoulizwa msimamo wake juu ya Ufaransa kupeleka silaha kwa Waasi amesema hatua hiyo itawafanya wananchi wazidi kuathirika kwani wao ndiyo watakumbwa na athari za vita.

Mapema Viongozi wa AU kwenye mkutano wao uliofanyika Mjini Addis Ababa, Ethiopia kwa kauli moja walilaani mashambulizi ambayo yanafanywa na Majeshi ya Kujihami ya Nchi za Magharibi NATO na kutaka yasitishwe mara moja.

 

 

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.