Pata taarifa kuu
MAREKANI-DRC-UCHUMI

Marekani yaweka vikwazo dhidi ya afisa wa juu katika jeshi la DRC

Wizara ya fedha nchini Marekani juma hili imetangaza kuwawekea vikwazo vya kiuchumi jenerali mmoja wa serikali ya DRC anayetuhumiwa kushirikiana na makundi ya waasi, vikwazo vilivyowalenga pia makamanda watatu wa makundi ya waasi mashariki mwa nchi hiyo.

Askari wa Tanzaniawakipokea miili ya walinda amani wa MONUSCO kutoka Tanzania waliuawa Beni, DRC.
Askari wa Tanzaniawakipokea miili ya walinda amani wa MONUSCO kutoka Tanzania waliuawa Beni, DRC. REUTERS/Emmanuel Herman
Matangazo ya kibiashara

Wizara ya fedha imesema kuwa Jenerali Muhindo Akili Mundos wa jeshi la DRC na mtu wa karibu wa rais Joseph Kabila amekuwa akijipatia faida kwa kushirikiana na makundi ya waasi Jimboni Kivu Kaskazini mwaka 2014 wakati alipotakiwa kufanya kazi pamoja na tume ya umoja wa Mataifa MONUSCO.

Taarifa ya Marekani imesema Mundos alishindwa kuingilia kati kuzuia vitendo vya utekaji nyara na mauaji, kusajili wapiganaji na kuwasaidia kwa vifaa vya kijeshi makamanda wa makundi ya waasi walioshiriki mauaji ya halaiki.

Marekani pia imewaweka kwenye orodha ya hatari mfungwa aliyetoroka Gedeon Kyungu Mutanga anayeongoza kundi la waasi wa Kata Katanga jimboni Katanga, Guidon Shimiray Mwissa aneyeongoza kundi la waasi wa Nduma Jimboni Kivu Kaskazini na Lucien Nzabamwita kiongozi wa kundi la waasi wa FDLR.

Vikwazo vya Marekani vimekuja baada ya mwishoni mwa juma lililopita Serikali ya Ufaransa nayo kutangaza kuzuia mali za jenerali wa jeshi la DRC aliyeko kwenye orodha ya vikwazo ya umoja wa Mataifa.

Katika hatua nyingine mzozo kati ya DRC na Serikali ya Ubelgiji umeendelea kuchukua sura mpya baada ya Serikali ya Kinshasa kuutaka utawala wa Brussels kupunguza karibu nusu ya safari za ndege zake zinazofanya safari kila wiki nchini humo.

Mamlaka ya usafiri wa anga ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imelitaka shirika la ndege la Brussels Airlines kuangalia upya ratiba ya safari ya ndege zake kuelekea Kinshasa.

Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya usafiri wa umma, Jean Tshiumba Mpunga, amesema mwanzoni shirika hilo lilikuwa likifanya safari zake mara saba kwa wiki, lakini sasa limetakiwa kupunguza safari zake kutoka saba hadi nne kwa wiki kuanzia jana Jumatatu.

Hatua hii inakuja baada ya serikali ya Kinshasa kutangaza kuwa itafunga ubalozi wake jijini Anvers Ubelgiji, na kuitaka Ubelgiji kufanya hivyo na kuwaondoa wafanyakazi wake.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.