Pata taarifa kuu
SOKA-FIFA

Rais wa zamani FIFA Joao Havelange aaga dunia

Rais wa zamani wa Shirikisho la soka duniani FIFA Joao Havelange, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 100.

Rais wa zamani wa FIFA Joao Havelange, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 100
Rais wa zamani wa FIFA Joao Havelange, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 100 José Cruz/ Agência Brasil (19/04/2010)
Matangazo ya kibiashara

Kifo cha raia huyo wa Brazil kimethibitishwa na uongozi wa Hospitali ya Samaritano jijini Rio de Janeiro alikokuwa amelazwa kutibiwa baada ya kuanza kusumbuliwa na ugonjwa wa pneumonia mwezi Julai.

Havelange, aliongoza FIFA kwa muda wa miaka 24 kati ya mwaka 1974 hadi 1998.

Atakumbukwa kuwa rais wa FIFA aliyeongoza Shirikisho hili kwa muda mrefu baada ya Mfaransa Jules Rimet aliyeongoza kwa muda wa miaka 33 kati ya mwaka 1921 ba 1954.

Pamoja na kuhudumu soka duniani kwa kipindi hicho, Havelange alihudumu pia katika Kamati ya Kimataifa ya Michezo ya Olimpiki kwa karibu miaka 50 kati ya mwaka 1963 hadi 2011.

Mwezi Aprili mwaka 2013 alijiuzulu kama rais wa heshima  wa FIFA baada ya kuzuka kwa madai ya ufisadi wakati wa uongozi wake.

Atakumbukwa sana kwa kuanzisha mashindano ya kombe la dunia kwa wachezaji wasiozidi miaka 17 na 20 miaka ya 80 na baadaye kombe la dunia la wanawake miaka 90.

Aidha, mchango wake utakumbukwa sana kuboresha usimamizi wa mchezo wa soka katika Makao Makuu mjini Zurich, baada ya kuingia madarakani wakati huo Ofisi hiyo ikiwa na wafanyikazi 12.

Pamoja na hayo, wakati wa uongozi wake aliongeza mataifa yanayoshiriki katika kombe la dunia kutoka 24 hadi 32 kuanzia mwaka 1998, na  bara la Afrika kupata nafasi mbili zaidi na kufikisha idadi ya mataifa matano yanayoshiriki katika kombe la dunia hadi sasa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.