Pata taarifa kuu
EURO 2016

Italia, Ureno na Sweden katika mtihani mkubwa kombe la Ulaya 2016

Mechi za kombe la mataifa ya Ulaya 2016, zinatarajiwa kuendelea tena Jumatano hii, kwa timu kutoka kundi E na F kupepetana katika kusaka timu ambazo zitafuzu na kuingia kwenye hatua ya 16 bora ya michuano ya mwaka huu.

Mshambuliaji wa Ureno, Christian Ronaldo anayepiga mpira akiwa na wenzake mazoezini, Ureno inacheza na Hungary.
Mshambuliaji wa Ureno, Christian Ronaldo anayepiga mpira akiwa na wenzake mazoezini, Ureno inacheza na Hungary. REUTERS/Darren Staples
Matangazo ya kibiashara

Mechi za kwanza zitakuwa ni zile za kundi F, ambapo Hungary watakuwa wakicheza na Ureno, huku timu ya taifa ya Iceland itakuwa ikicheza na Austria kwenye mechi ambazo ni muhimu kwa timu zote kushinda ili kujikatia tiketi ya kusonga mbele hatua inayofuata.

Hungary ambayo inaongoza kundi lake ikiwa na alama 4, itaingia uwanjani kwa lengo moja tu la kuhakikisha inafanya kila linalowezekana ili imalize kwenye nafasi ya kwanza kutoka kundi lake, na hilo litawezekana ikiwa itaifunga Ureno ama kutoka sare.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Ureno wakiwa kwenye mazoezi ya pamoja kuelekea mchezo wao na Hungary.
Wachezaji wa timu ya taifa ya Ureno wakiwa kwenye mazoezi ya pamoja kuelekea mchezo wao na Hungary. REUTERS/Christian Hartmann

Timu ya taifa ya Ureno inayoongozwa na nahodha, Christian Ronaldo, itaingia uwanjani na yenyewe ikiwa na nia moja ya kuhakikisha inapata ushindi kwenye mechi yake dhidi ya Hungary, ushindi ambao utaifanya timu hiyo pengine imalize kwenye nafasi ya kwanza kutoka kundi F.

Ronaldo ambaye mpaka sasa hajafunga bao lolote kwa timu yake, anakosolewa kwa sehemu kubwa na wachambuzi wa masuala ya soka, wanaoona kuwa mchezaji huyo anacheza kibinafsi kwenye timu, ubinafsi ambao hauisaidii timu yake zaidi ya kuiwekea mazingira magumu zaidi ya kufuzu.

Mlinda mlango wa timu ya taifa ya Hungary, Gabor Kiraly.
Mlinda mlango wa timu ya taifa ya Hungary, Gabor Kiraly. REUTERS/Jason Cairnduff

Mchezo wa leo ni muhimu kwa timu ya taifa ya Ureno ikiwa inataka kusonga mbele kwenye hatua inayofuata, kwa kua hata ikipata sare huenda matokeo hayo yasiisaidie sana timu hiyo kwakuwa itategemea mchezo kati ya Iceland na Austria.

Iceland yenyewe inaingia uwanjani ikiwa na alama 2 sawa na Ureno lakini zikitofautiana kwa magoli ya kufunga na kufungwa, na itakuwa inacheza na Iceland yenye alama moja kwenye kundi lake, huku ikihitaji ushindi ili nayo iweze kufuzu kwenye hatua inayofuata.

Wachezaji wa Austria wakiwa mazoezini.
Wachezaji wa Austria wakiwa mazoezini. REUTERS/Lee Smith

Timu ya Iceland inahitaji ushindi kwenye mchezo wake dhidi ya Austria ikiwa inahitaji kumaliza ya kwanza kwenye kundi lake, lakini itabidi ifanye kazi ya ziada kuifunga Austria ambayo na yenyewe inahitaji ushindi kwenye mchezo wake ili ikate tiketi na kuingia kwenye hatua ya 16 bora.

Mechi zote za kundi F ni muhimu kwa kila timu, kwakua ikiwa mmoja kati yao atapoteza mchezo wake atakuwa anatoa nafasi kwa wengine kukata tiketi na kuingia kwenye hatua ya 16 bora.

Dakika 90 za mchezo ndizo zitakazoamua hatma ya kundi hili.

Katika kundi E, pia kutakuwa na mechi zitakazochezwa ambapo, timu ya taifa ya Italia itakuwa na kibarua dhidi ya timu ya taifa ya Jamhuri ya Ireland, huku huku Sweden yenyewe itakuwa na kibarua dhidi ya timu ya taifa ya Ubelgiji.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Italia wakifanya mazoezi kabla ya mechi yao na Ireland.
Wachezaji wa timu ya taifa ya Italia wakifanya mazoezi kabla ya mechi yao na Ireland. REUTERS/Vincent Kessler

Timu ya taifa ya Italia inaingia kwenye mchezo huu ikiwa tayari imeshakata tiketi ya kucheza hatua ya 16 bora, ikiwa na alama 6, ikifuatiwa na Ubelgiji yenye alama 3, huku Sweden na Jamhuri ya Ireland zenyewe zikiwa na alama moja moja.

Jamhuri ya Ireland yenyewe itakuwa inahitaji ushindi kuliko kuambulia sare kwenye mchezo wake dhidi ya Italia, ikiwa timu hii inataka kuingia kwenye hatua ya mtoano.

Ikiwa itapata ushindi dhidi ya Italia, Ireland itakuwa imefikisha alama 4 na hivyo kujiweka kwenye mazingira mazuri zaidi ya kucheza hatua ya kumi na sita bora ya michuano ya kombe la Ulaya mwaka huu.

Ubelgiji ambayol yenyewe haikuanza vema mchezo wake wa kwanza, itaingia uwanjani kucheza na Sweden huku ikiwa na alama tatu, ikihitaji ushindi dhidi ya Sweden, kama inataka kusonga mbele kucheza hatua ya 16 bora.

Mshambuliaji wa kimataifa wa timu ya taifa ya Sweden, Zlatan Ibrahimovic.
Mshambuliaji wa kimataifa wa timu ya taifa ya Sweden, Zlatan Ibrahimovic. REUTERS/Eric Gaillard

Sweden yenyewe yenye alama moja kwenye kundi lake, itakuwa ikimtegemea mchezaji Zlatan Ibrahimovic ambaye ni nahodha pia wa timu hiyo, ili aivushe kuingia hatua ya 16 bora, kwenye mchezo ambao ni wakufa au kupona kwa timu zote mbili.

Ikiwa Sweden itapoteza mchezo wa leo dhidi ya Ubelgiji, na Jamhuri ya Ireland ikashinda mchezo wake dhidi ya Italia, ni wazi kuwa timu hiyo itakuwa imeaga rasmi mashindano ya mwaka huu, kwahivyo mchezo wa leo ni muhimu sana kwa timu zote za kundi E.

Mechi kati ya Hungary na Ureno na Iceland dhidi ya Austria, zitaanza kuchezwa kwa pamoja maajira ya saa moja kamili za usiku kwa saa za hapa Afrika Mashariki, wakati Italia dhidi ya Jamhuri ya Ireland na Sweden dhidi ya Ubelgiji, wao watacheza maajira ya saa nne usiku kwa saa za hapa Afrika Mashariki.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.