Pata taarifa kuu
MAN CITY-GUARDIOLA-PELLEGRINI

Guardiola kuwa kocha wa Man City msimu ujao, je ataweza changamoto za ligi kuu ya Uingereza

Klabu ya Manchester City ya Uingereza, jumatatu ya wiki imefanya mapinduzi ya kushtukia katika soka baada ya kumtangaza Pep Guardiola kuwa kocha wao mkuu kwenye msimu ujao wa ligi kuu baada ya kumuwinda kocha huyu kwa miaka minne.

Pep Guardiola, kocha wa Bayern Munich ambaye sasa amesaini mkataba wa miaka 3 na klabu ya Manchester City
Pep Guardiola, kocha wa Bayern Munich ambaye sasa amesaini mkataba wa miaka 3 na klabu ya Manchester City Reuters/Fabian Bimmer
Matangazo ya kibiashara

Kocha Pep Guardiola ambaye ataachana na klabu yake ya Bayern Munich mwishini mwa msimu, atachukua nafasi ya kocha Manuel Pellegrini kwa mkataba wa miaka mitatu kwa mshahara unaotajwa kufikia paundi za Uingereza milioni 15 kwa mwaka.

Licha ya kuwa klabu ya Manchester City bado iko kwenye nafasi ya kutwaa mataji manne msimu huu, likiwemo taji la klabu bingwa ulaya na lile la ligi kuu ya Uingereza, Manuel Pellegrini anasema anafahamu kuwa wamiliki wa klabu hiyo walikuwa kwenye mazungumzo na Guardiola na yeye binafsi aliunga mkono kabla ya uteuzi.

Tangazo hili limefanya hata kuzima mihemko iliyokuwepo hapo awali ya klabu hiyo kusajili mchezaji mwingine katika muda wa mwisho wa dirisha dogo.

Pep Guardiola, kocha mkuu  wa Beyern Munich ambaye msimu ujao atajiunga na Manchester City
Pep Guardiola, kocha mkuu wa Beyern Munich ambaye msimu ujao atajiunga na Manchester City Reuters/Lukas Barth

Klabu ya Manchester City inayomilikiwa na Sheikh Mansour bin Zayed al-Nahyan, ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa kwa miezi kadhaa wamekuwa kwenye mazungumzo ya mwisho ya kukamilisha taratibu nyingine kabla ya Guardiola kuwa kocha mkuu wa timu hiyo katika msimu wa mwaka 2016-17.

Taarifa yake ilisema kuwa mkataba wake ni wa miaka mitatu, na kwamba majadiliano yalianza miaka minne iliyopita.

Imeongeza kuwa kama heshima kwa kocha Manuel Pellegrini na wachezaji, timu inapenda kuweka suala hili wazi ili kuondoa minong'ono ambayo ingeweza kuathiri mwenendo wa timu.

Wachambuzi wa masuala ya soka wanasema kuwa licha ya umahiri wa kocha Guardiola, kocha huyo atakumbana na upinzani mkali kwenye ligi kuu ya Uingereza ambayo imekuwa sio rahisi sana kwa makocha wengi wa kigeni.

Wengi wanasema kuwa huenda akafundisha msimu mmoja na kuachana na timu hiyo, kwakuwa timu nyingi za Uingereza zinaamini katika mafanikio ya haraka, na hazina uvumilivu sana ikiwa kocha atavurunda katika msimu wa kwanza.

Wapo wanaoona kuwa kulinga na kikosi chenyewe cha City kilivyo, huenda Guardiola akakisuka vizuri zaidi na kutwaa mataji zaidi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.