Pata taarifa kuu
RONALDO-LIM-PICHA

Bilionea, Peter Lim anunua haki miliki ya picha za Christian Ronaldo

Bilionea Peter Lim, raia wa Singapore na mmiliki wa klabu ya mpira wa miguu ya nchini Uhispania, Valencia, ameendelea kujipambanua kwenye ulimwengu wa masoko ya michezo, baada ya kutangaza kununua haki miliki ya picha za mshambuliaji wa Real Madrid, Christian Ronaldo.

Bilionea, Peter Lim ambaye sasa amenunua haki miliki ya matangazo ya picha za Ronald
Bilionea, Peter Lim ambaye sasa amenunua haki miliki ya matangazo ya picha za Ronald Reuters
Matangazo ya kibiashara

Kampuni ya masuala ya Habari ya Mint yenye makao yake makuu jijini Hong Kong na inayimilikiwa na Lim, imetangaza kwenye mtandao wake kuwa, mchezaji huyo ameingia mkataba wa miaka sita na kampuni hiyo ambapo sasa itashuhudiwa mchezaji huyo akitangazwa zaidi barani Asia.

Chini ya mkataba huu mpya, kampuni ya Mint Media itamiliki na kusimamia haki zote za picha za Ronaldo ukiacha zile ambazo zinatumiwa na klabu yake ya Real Madrid ya Uhispania.

Christiano Ronaldo akiwa na tuzo yake ya mchezaji bora wa dunia wa FIFA
Christiano Ronaldo akiwa na tuzo yake ya mchezaji bora wa dunia wa FIFA Facebook Fifa Ballon d'Or

Ronaldo ambaye amepata umaarufu mkubwa kutokana na kusaini mikataba mbalimbali ya matangazo, anatajwa na Jarida la Forbes kuwa ni mchezaji wa tatu, ghali zaidi na anayelipwa fedha nyingi kama mwanamichezo kwa mwaka 2015 baada ya mwanamasumbwi, Floyd Mayweather wa Marekani na bondia wa Ufilipino, Manny Pacquiao.

"Ronaldo sio tu mchezaji soka bora, lakini pia ni mtu maarufu. Sina shaka na nina imani kuwa matangazo ya Christian Ronaldo yataendelea kukua." Alisema Lim kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Ronaldo mwenyewe amemuelezea Lim kama rafiki yake wa karibu na hakuficha hisia zake kwa namna anavyompenda mfanyabiashara huyu bilionea.

Ronaldo ameongeza kuwa "Naamini atakuwa mshirika mzuri na mtu mwenye thamani katika matangazo yangu." alimaliza mchezaji bora mara tatu wa dunia wa FIFA.

Ronaldo amejiwekeza na amekuwa maarufu zaidi katika mitandao ya kijamii ambapo anamashabiki milioni 36 duniani kwenye mtandao wa Twitter na mashabiki milioni 103 kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.

Lim, aliyewahi kuwa muuza hisa, mwaka uliopita alinunua hisa na kuwa mmiliki wa klabu ya Valencia ya Uhispania, lakini pia ni mwekezaji muhimu katika kampuni ya McLaren.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.