Pata taarifa kuu
LIGI KUU YA UINGEREZA

Chelsea yazima ndoto za Man Utd kutetea taji lake msimu huu

Matumaini ya timu ya Manchester United ya nchini Uingereza kutetea taji lake la ligi kuu ya nchi hiyo yameendelea kutoweka kufuatia kipigo ilichopata timu hiyo toka kwa vijana wa kocha Josee Mourinho, klabu ya Chelsea. 

Mshambuliaji wa Chelsea, Samwel Etoo akiifungia bao la tatu na la ushindi timu yake hapo jana
Mshambuliaji wa Chelsea, Samwel Etoo akiifungia bao la tatu na la ushindi timu yake hapo jana Reuters
Matangazo ya kibiashara

Ushindi wa timu ya Chelsea hapo jana ikiwa nyumbani kwenye uwanja wake wa Stamford Bridge umeifanya timu kusogea hadi kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo kwa kujikusanyia alama 49 nyuma ya Manchester City na Arsenal.

Mshambuliaji wa kimataifa raia wa Cameroon, Samwely Etoo ndiye aliyepeleka kilio kwa vijana wa David Moyes kwa kupachika mabao yote matatu katika dakika ya 17, 45 na 49 kipindi cha pili.

Kwenye mchezo huo ambao Manchester United waliuanza vizuri na kila mtu kuanza kuamini pengine wangeweza kuibuka na ushindi, hali haikuwa hivyo kwani dakika ya 17 ya mchezo Etoo aliiandikia bao la kuongoza timu yake kabla ya kupachika bao la pili kabla ya mapumziko.

Kipindi cha pili mambo hayakubalika sana licha ya mabadiliko ya harakaharaka yaliyofanywa na Moyes kutaka kurejesha mabao hayo, lakini wakati timu yake ikijitahidi kushambulia uzembe wa mabeki ulimpa nafasi tena Etoo kupachika bao la 3 katika dakika ya 49 ya kipindi cha pili kabla ya Javier Hernandez kuipatia bao la kufutia machozi timu yake katika dakika ya 78 kipindi cha pili.

Mara baada ya mchezo huo, kocha wa Manchester United, David Moyes amekiri timu yake msimu huu kufanya vibaya na kwamba haridhishwi na wala hafurahii kuona timu yake ikiboronga kiasi hichi hali inayomfanya awe kwenye wakati mgumu.

Kwa matokeo ya hapo jana ni wazi sasa Manchester United haipewi nafasi tena ya kutetea taji lake na sasa itawania nafasi ya nne ili walau ipate nafasi ya kucheza klabu bingwa ulaya.

Kwenye mechi nyingine timu ya Swansea ilikuwa nyumbani kwenye uwanja wake wa Liberty kuwakaribisha Tottenham kwenye mchezo ambao umeshuhudia Swansea wakipoteza mchezo huo kwa kukubali kichapo cha mabao 3 kwa moja huku mabao mawili ya Tottenham yakifungwa na Emmanuel Adebayor mshambuliaji wa kimataifa kutoka Togo.

Kwasasa timu ya Arsenal inaongoza kwenye msimamo wa ligi kwakuwa na alama 51 wakifuatiwa na Manchester City wenye alama 50, Chelsea wanaalama 49 huku Liverpool wakifuatia wakiwa na alama 43 sawa na timu ya Tottenham huku Manchester United wakisalia kwenye nafasi ya 7 wakiwa na alama 37.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.