Pata taarifa kuu
SOKA

Kocha wa Zambia Herve Renard aruhusiwa kuondoka

Shirikisho la soka nchini Zambia FAZ limetangaza kuwa kimempa nafasi ya kuondoka kocha wa timu ya taifa ya Chipolopolo Mfaransa Herve Renard.

Matangazo ya kibiashara

Renard alianza kuifunza Zambia mwaka 2008 na akaondoka mwaka 2010 kabla ya kurejeshwa tena mwaka 2011 na kuiongoza Chipolopolo kunyakua taji la klabu bingwa barani Afrika mwaka 2012 nchini Gabon.

Hata hivyo, Renard alishindwa kutetea taji hilo wakati wa michuano hiyo mapema mwaka huu nchini Afrika Kusini na pia akashindwa kuifikisha Zambia katika mzunguko wa mwisho wa kufuzu kwa kombe la dunia nchini Brazil mwaka ujao.

Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 45 sasa atakuwa kocha wa klabu ya Sochaux nyumbani kwao inayoshiriki katika ligi ya klabu bingwa nchini Ufaransa.

Msemaji wa FAZ Eric Mwanza amesema kuwa chama hicho kimezungumza na Herve na wakakubaliana kuwa hakuna tatizo lolote la yeye kuacha kazi kama kocha wa timu ya Zambia.

Aidha, FAZ imesema kuwa ni fahari kubwa sana kwa Herve anayefanya kazi barani Afrika kutafutwa na klabu kubwa ya soka barani Ulaya jambo ambalo amesema inaonesha wazi kuwa soka la Zambia linatambulika na ukufunzi wa  Renard ni wa kimataifa.

Baada ya kuondoka kwa Renard, kocha msaidizi Patrice Beaumelle sasa ataingoza Chipololo kujiandaa kucheza na Brazil katika mchuano wa Kimataifa wa kirafiki wiki ijayo mjini Beijing nchini China.

Kabla ya kuanza kuifunza Zambia, Renard pia aliwahi kuhudumu kama kocha msaidizi wa Ghana chini ya kocha Claude Leroy.

Renard pia amewahi kuwa kocha Angola kabla ya kurejea Zambia.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.