Pata taarifa kuu
ISRAEL

Israel: Netanyahu asalimu amri, akubali kuitisha uchaguzi mkuu mwingine

Bunge la Israel Alhamisi hii limepiga kura kuruhusu kufanyika kwa uchaguzi mkuu mpya baada ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu kushindwa kuunda Serikali na vyama vingine.

Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu. MENAHEM KAHANA / AFP
Matangazo ya kibiashara

Uamuzi wa bunge umekuja ikiwa ni mwezi mmoja tu umepita tangu nchi hiyo ifanye uchaguzi wake mkuu, ulioshuhudia waziri mkuu Netanyahu na chama chake cha Likud wakishindwa kupata ushindi wa jumla kuwawezesha kuunda Serikali.

Hatua hii imekuja pia baada ya muda wa mwisho aliokuwa nao waziri mkuu Netanyahu kuunda Serikali, kupita baada ya majuma kadhaa ya mazungumzo na vyama vingine kugonga mwamba.

Uamuzi wa waziri mkuu Netanyahu kukubali kutisha uchaguzi mkuu mwingine, kumezuia rais Reuven Rivlin kuchagua mtu mwingine kujaribu kuunda Serikali, lakini hata hivyo uamuzi wake unazidisha sintofahamu zaidi ya mustakabali wake kisiasa.

Haya yanajiri wakati huu waziri mkuu Netanyahu anapambana kusafisha jina lake kutokana na kashfa za rushwa, ambapo tayari kulikuwa kumeanza mchakato wa chini kwa chini kujaribu kumuondoa madarakani.

Mwezi Julai mwaka huu waziri mkuu Netanyahu anatarajiwa kuwa waziri mkuu wa kwanza aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi, akiipita rekodi ya muasisi wa taifa hilo David Ben-Gurion.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.