Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia inasema kuwa uhalifu huo hauendani kabisa na sera za utawala wa kifalme.
"Saudi Arabia inafutilia mbali msimamo uliotolewa na bunge la Seneti la Marekani ambalo kupitia habari zisizokuwa na msingi na ambazo zinaingilia kati katika masuala ya ndani ya nchi hii, kudhoofisha jukumu lake katika kanda na kimataifa," imesema taarifa ya wizara hiyo iliyochapishwa na shirika la Habari la Saudia.
"Tangu awali Saudi Arabia imehakikishia kwamba mauaji ya raia wa Saudia Jamal Khashoggi ni uhalifu mbaya ambao hauendani na sera ya utawala wa kifalme au taasisi zake."
Siku ya Alhamisi bunge la Seneti la Marekani lilimtaka Rais Donald Trump kutambua Mwanamfalme wa Saudi Arabia kuwa alihusika katika mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi na kupigia kura azimio ambalo linaomba kusitishwa misaada ya kijeshi kwa utawala wa Saudi Arabia.