Pata taarifa kuu
PAKISTAN-MALALA

Malala Yousafzai azuru Pakistan kwa mara ya kwanza

Mshindi wa tuzo la Nobel Malala Yousafzai amerejea nchini Pakistan kwa mara ya kwanza tangu apigwe risasi na wapiganaji wa kundi la Taliban miaka 6 iliyopita kwa kuhamasisha wasichana kupata elimu.

Msichana na mwanaharakati wa elimu na mshindi wa tuzo la Nobel, Malala Yousafzai.
Msichana na mwanaharakati wa elimu na mshindi wa tuzo la Nobel, Malala Yousafzai. REUTERS/Darren Staples
Matangazo ya kibiashara

Malala mwenye umri wa miaka 20 amefanya ziara ya kushtukiza akiwa na wazazi wake chini ya ulinzi mkali kwenye uwanja wa ndege wa Islamabad ambapo mitandao ya kijamii ilifurika salamu za pongezi huku baadhi wakimkosoa.

Malala anaheshimiwa kidunia kwa harakati zake lakini maoni yamegawanyika nchini Pakistan ambako baadhi ya watu wenye misimamo wanamuona kama kibaraka wa nchi za magharibi aliye katika misheni ya kuichafua nchi yao.

Mwanaharakti huyu wa elimu anatarajiwa kukutana na waziri mkuu Shahid Khaqan Abbas katika ziara yake ya siku nne nchini Pakistan.

"Atakutana na watu kadhaa akiwa hapa lakini ratiba yake haijawekwa wazi kwa sababu za kiusalama," amesema msemaji wa wizara ya mambo ya nje Muhammad Faisal.

"Tunamkaribisha Malala....amerudi nyumbani. Ni uelekeo chanya," alisema msemaji huyo akimuita Malala "mmoja wa wasichana wadogo na mwenye ujasiri," akiongeza kuwa wananchi wa Pakistana wanapaswa kumuheshimu.

Wakazi wengi wa bonde la Swat ambako Malala aliishi maisha yake yote kabla ya kushambuliwa na wapiganaji wa Taliban, wamefurahia ujio wake.

"Sikuwahi kufikiri kuwa anaweza kurejea tena," alisema Rida Siyal mwanafunzi ambaye amedai Malala alikuwa rafiki yake kabla ya shambulio la risasi.

Ahmad Shah ambaye amesema alikuwa rafiki wa baba yake amemuita Malala kama nembo ya ushujaam na kuongeza kuwa alitakiwa kurejea nyumbani mapema zaidi.

Malala amekuwa nembo ya dunia kwa harakati za kutetea haki za binadamu baada ya mpiganaji wa Taliban kushambulia basi lililokuwa limewabeba wanafunzi kwenye mji wa Swat Octoba 9, 2012, ambapo aliuliza Malala ni nani na kisha kumfyatulia risasi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.