Pata taarifa kuu
MAREKANI-SYRIA-URUSI

Urusi huenda ikaifanya Marekani kutekeleza mashambulizi nchini Syria

Mapendekezo mawili ya Marekani kuhusu kuchukua hatua za kusitisha mapigano nchini Syria kwenye baraza la usalama la umoja wa Mataifa huenda likaifanya nchi ya Urusi kutumia kura yake ya turufu kuzuia azimio lolote, hatua ambayo wanadiplomasia wanasema kuna uwezekano Marekani ikatekeleza mashambulizi nchini Syria.

Uharibufu katika mji wa Mashariki mwa Ghouta nchini Syria kutokana na vita vinavyoendelea
Uharibufu katika mji wa Mashariki mwa Ghouta nchini Syria kutokana na vita vinavyoendelea REUTERS/Bassam Khabieh
Matangazo ya kibiashara

Nchi ya Urusi imetumia kura yake ya turufu mara 11 kuzuia maazimio yanayoilenga nchi ya Syria na kumlinda rais Bashar al-Asad dhidi ya vikwazo, uchunguzi wa makosa ya kivita na matumizi ya silaha za kemikali.

Tayari kumeibuka wasiwasi kuwa huenda Urusi ikatumia kura yake ya 12 ya turufu baada ya Marekani juma hili kuwasilisha pendekezo jingine la usitishaji wa mapigano kwa siku 30 mashariki mwa mji wa Ghouta, ngome ya upinzani inayosalia.

Hatua ya Marekani ilitokana na kushinidikana kutekelezwa kwa azimio la Umoja wa Mataifa la kusitisha mapigano ili kupelekwa kwa misaada ya kibinadamu kwenye mji huo licha ya kuwa liliungwa mkono na Urusi inayovisaidia vikosi vya Serikali kutekeleza mashambulizi kwenye mji huo.

Juma hili Marekani imetishia kuwa italazimika kuchukua hatua dhidi ya Syria ikiwa mapigano yataendelea.

Waangalizi wa mzozo wa Syria wanasema kwa karibu miezi miwili pekee watu zaidi ya elfu moja wamepoteza maisha Mashariki mwa Ghouta pekee huku maelfu wakiwa hatarini ya kupoteza maisha kwa ukosefu wa mahitaji muhimu kama dawa na chakula.

Serikali ya Syria inasema vita vitaendelea hadi pale mji huo utakapokombolewa.

Vita nchini Syria vinaingia mwaka wa nane siku ya Alhamisi.

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.