Upinzani nchini Syria wakataa mazungumzo ya amani yaliyopangwa na Urusi
Muungano wa upinzani nchini Syria umesema hautashiriki katika mazungumzo ya amani yaliyoandaliwa na Urusi.
Imechapishwa:
Hili ni pigo kwa serikali ya Urusi ambayo imekuwa ikijaribu kuwashawishi wapinzani kuja kwenye meza ya mazungumzo.
Mazungumzo hayo yalikuwa yamepangwa kufanyika wiki ijayo mjini Sochi, yakiongozwa na Urusi ambayo imekuwa ikiisaidia serikali ya rais Bashar Al Assad kupambana na waasi.
Upinzani nchini Syria umesema, baada ya mashauriano ya kina pamoja na wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na nchi nyingine, hawajaridhishwa na hatima ya mazungumzo hayo.
Makundi mengine ya waasi ambayo yapo kwenye upinzani nchini Syria nayo yamekataa kushiriki katika mazungumzo hayo.
Mbali na mazungumzo haya yaliyokuwa yamepangwa na Urusi, Umoja wa Mataifa umekuwa ukijaribu pia kupatanisha pande zote mbili bila mafanikio.
Siku ya Ijumaa, msuluhishi wa mzozo huu Staffan de Mistura alishindwa kuafikiana na wawakilishi wa serikali na upinzani, katika mazungumzo mengine yaliyokuwa yanaendelea mjini Vienna nchini Austria.
Mzozo nchini Syria umeendelea kwa mwaka wa saba sasa na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 300,000 na mamilioni kuyakimbia makwao.