Putin agiza sehemu moja ya askari wake kuondoka Syria
Rais wa Urusi Vladimir Putin ameamuru kuondolewa kwa sehemu ya kikosi cha wanajeshi wa nchi yake ambao wamekuwa wakipambana na waasi nchini Syria.
Imechapishwa:
Putin ametoa agizo hilo baada ya ziara yake ya kushtukiza nchini Syria katika jimbo la Latakia, alikopokelewa na rais Bashar al-Assad.
Hatua hii imekuja baada ya Urusi hivi karibuni kusema kuwa, ilikuwa imemaliza kazi yake nchini Syria baada ya kulemewa kwa wapiganaji wa Islamic State.
Rais Bashar, alikuwa nchini Urusi hivi karibuni na kumshukuru rais Putin kwa kulisaidia taifa lake.
Jeshi la Urusi limekuwa nchini Syria tangu mwaka 2015, baada ya kuombwa na serikali ya Damascus kusaidia katika makabiliano na waasi wanaopinga serikali ya rais Assad.
Zaidi ya watu 340,000 wameuwawa nchini Syria tangu mwezi Machi mwaka 2011 ulipoibuka mgogoro, uliopelekea serikali kupambana na makundi ya kigaidi pamoja na ya waasi.