Pata taarifa kuu
IRAQ-MAREKANI-ISIL

Washirika wa Marekani Iraq wakiri huenda walihusika na mauaji ya raia Mosul

Muungano unaoongozwa na Marekani kwenye mashambulizi dhidi ya wanajihadi unasema kuwa huenda mashambulizi yaliyofanywa juma lililopita na kuua mamia ya raia, yalitekelezwa kimakosa na Marekani.

Moshi mkubwa ukionekana kwenye anga ya mji wa Mosul.
Moshi mkubwa ukionekana kwenye anga ya mji wa Mosul. REUTERS/Suhaib
Matangazo ya kibiashara

Kauli ya muungano huo inatolewa wakati huu ambao umoja wa Mataifa na shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International wakitaka kufanyike juhudi za kina kuwalinda raia dhidi ya mashambulizi.

Mamia ya raia bado wamenaswa kwenye mji wa West Mosul, ambapo wamejikuta kwenye mapigano kati ya wanajihadi wa kiislamu na vikosi vya Serikali ya Iraq ambavyo vinasaidiwa na majeshi ya nchi washirika na Marekani.

Mji wa West Mosul ni mdogo na unakaliwa na raia wengie zaidi ukilinganisha na mji wa Mashariki, hii ikiwa na maana kuwa mashambulizi yoyote yanayofanyika yanawaweka raia hao kwenye hatari kubwa.

“Kuna uwezekano mkubwa kuwa tulihusika kwenye mauaji dhidi ya raia,” alisema Luteni jenerali Stephen Townsend, kamanda wa vikosi vinavyoongozwa na Marekani kwenye operesheni dhidi ya kundi la Islamic State.

“Ikiwa raia wale wasio na hatia waliuawa, basi kilikuwa ni kitendo ambacho hakikukusudiwa kwenye vita hii,” alisema kamanda huyo.

Townsend ameeleza makabiliano kwenye mji huo kama makabiliano ambayo ni muhimu sana kwa wakati huu toka pengine kumalizika kwa vita ya pili ya dunia na pengine ni vita ngumu zaidi kupiganwa.

Tayari muungano huo ulishakiri kuwa ulitekeleza mashambulizi Machi 17 mwaka huu kwenye mji huo ambako mamia ya raia waliripotiwa kuuawa na kwamba wamefungua uchunguzi rasmi.

Nchi ya Iraq pia inafanya uchunguzi kuhusiana na tukio hilo lakini inaonekana kuitupia lawama Marekani.

Msemaji wa tume ya haki za binadamu ya umoja wa Mataifa Ravina Shamdasani, amesema juma hili kuwa watu zaidi ya 300 wameuawa kwenye mji huo toka Februari 17 mwaka huu.

Kundi la Islamic State limekuwa likitumia raia kama kinga ya mashambulizi toka kwa nchi washirika na Marekani na vikosi vya Iraq.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.