Upinzani wa Syria waituhumu Serikali kutaka kukwamisha mazungumzo yanayoendelea
Muungano wa upinzani wa Syria unaoshiriki kwenye mazungumzo ya kusaka suluhu mjini Geneva, wanautuhumu utawala wa Damascus kwa makusudi kujaribu kukwamisha mazungumzo yanayoendelea, baada ya mpatanishi mkuu wa mzozo huo kuzitaka pande zote kujiepusha na mashambilizi zaidi, ambapo amelaani shambilio la mwishoni mwa juma kwenye mji wa Homs.
Imechapishwa:
Kamati ya juu ya majadiliano ya upinzani, imetoa kauli hiyo baada ya mwakilishi wa Serikali balozi Bashar al-Jaafari kusema kuwa ikiwa mpinzani yeyote hatalaani shambulio la kwenye mji wa Homs, watawahesabu kama magaidi.
Upinzani huo unasema kuwa, utawala wa Syria kwa makusudi kabisa hataki nchi hiyo ipate suluhu ya kisiasa na kwamba balozi Jaafari anajaribu kupindisha kile kilichowapeleka mjini Geneva.
Wapinzani wanasema toka kwenye mazungumzo ya awali yaliyofanyika mjini Geneva, neno pekee ambalo utawala wa Damascus unalijua ni "ugaidi".
Mjumbe maalumu wa umoja wa Mataifa, Staffan de Mistura alianzisha mazungumzo mengine ya raundi ya nne mjini Geneva alhamisi ya wiki iliyopita, na kama ilivyoshuhudiwa kwenye mikutano iliyopita ni wazi kumekuwa na hatua ndogo sana ambazo zimepigwa kwenye mazungumzo haya.
Shambulio la kwenye mji wa Homs mwishoni mwa juma, lililenga vituo viwili vya kijeshi, ambapo mamia ya watu waliuawa akiwemo mkuu wa intelijensia wa vikosi vya rais Assad.
Ujumbe wa Serikali unaoshiriki mazungumzo mjini Geneva, umepa kutofumbia macho shambulio la mwishoni mwa juma na kuapa kulipa kisasi, hali ambayo tayari imeanza kushuhudiwa kwa vikosi vya Serikali kutekeleza mashambulizi ya anga mfululizo.