Pata taarifa kuu
KENYA-MOI-SIASA

Wakenya waendelea kuomboleza kifo cha Moi

Wakenya wanaendelea kuomboleza kifo cha rais wa pili wa Kenya Daniel Torotich Arap Moi , aliyefariki dunia Jumanne wiki hii katika hospitali ya jijini Nairobi.

Daniel Arap Moi, Rais wa zamani wa Kenya (kulia), hapa ilikuwa Disemba 28, 2002, muda mfupi kabla ya kuondoka madarakani.
Daniel Arap Moi, Rais wa zamani wa Kenya (kulia), hapa ilikuwa Disemba 28, 2002, muda mfupi kabla ya kuondoka madarakani. ALEXANDER JOE / AFP
Matangazo ya kibiashara

Maombolezo ya kitaifa yanaendelea nchini Kenya hadi rais huyo wa zamani aliyeongoza nchi hiyo kwa miaka 24 atakapozikwa.

Wakati huo huo viongozi mbalimbali barani Afrika wameendelea kutuma risala za rambi rambi kwa wananchi wa Kenya, kufuatia kifo cha rais wao wa zamani.

Moi alikuwa kiongozi muhimu barani Afrika na katika ukanda wa Afrika Mashariki na rais wa Tanzania John Magufuli amesema rais huyo wa zamani atakumbukwa kwa jitihada zake za kuimarisha jumuiya ya Afrika Mashariki.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni, alishirikiana kwa karibu na Moi, katika harakati za kufufua Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Daniel Torotich Arap Moi aliyeongoza Kenya kwa miaka 24, kabla ya kustaafu mwaka 2002, amekuwa akiumwa kwa muda wa kipindi kirefu. Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 95.

Daniel Torotich Arap Moi, alikuwa rais aliyeongoza Kenya kwa muda mrefu katika historia ya nchi hiyo, kati ya mwaka 1978 hadi 2002.

Alichukua hatamu ya uongozi wa nchi kutoka kwa rais wa kwanza wa nchi hiyo Jomo Kenyatta baada ya kufariki dunia mwaka huo wa 1978, na atakumbukwa sana kwa umahiri wa kisiasa akiongoza chama tawala wakati huo cha Kanu.

Wakati wa uongozi wake, Moi, alipewa jina la Baba Moi, kwa sababu alipendwa na wananchi wa kawaida, hasa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwa kuagiza wapewe maziwa mara kwa mara, yaliyofahamika kama maziwa ya Nyayo.

Hata hivyo, kwa mataifa ya Magharibi na wapinzani wake, aliongoza Kenya kwa mkono wa chuma, huku wakosoaji wake wakisema uongozi wake ulikiuka haki za binadamu na kuongezeka kwa kashfa za ufisadi.

Mwaka 1992, Moi alikubali mabadiliko ya katiba baada ya shinikizo, kutoka ndani na nje ya nchi hiyo na kukubali kuwepo kwa vyama vingi.

Hadi kifo chake, waliokosoa uongozi wake, wanamkumbuka kama kiongozi ambaye alikuwa dikteta aliyekataa kuondoka madarakani, lakini kwa waliompenda, wanamkumbuka kama kiongozi aliyehuburi amani na upendo na kuyasaidia mataifa jirani.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.