Pata taarifa kuu
BURUNDI-USALAMA

Rais wa Burundi ahusishwa kwa ukiukwaji wa haki za binadamu

Kamati ya Umoja wa Mataifa inayochunguza visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Burundi, inasema rais Pierre Nkurunziza amekuwa akihusika katika ukiukwaji wa haki za binadamu.

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza Juni 7, 2018.
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza Juni 7, 2018. REUTERS/Evrard Ngendakumana
Matangazo ya kibiashara

Kamati hiyo imewasilisha ripoti yake katika tume ya Umoja wa Mataifa inayishughulikia haki za binadamu yenye makao yake jijini Geneva nchini Uswizi.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa, wanasiasa wa upinzani na watu wengine ambao hawashirikiani na serikali kuelekea Uchaguzi wa mwaka 2020, wameuawa au kutekwa.

Serikali ya Burundi imekanusha ripoti hiyo na kusema imechochewa kisiasa.

Hivi karibuni Tume ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Burundi ilibaini katika ripoti yake kwamba "hali ya hofu" inatawala katika nchi hiyo, ikiwa imesalia miezi minane kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

Katika ripoti yake, Tume ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Burundi, iliyoundwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 2016, ilielezea jinsi mamlaka nchini humo na vijana wa chama tawala, Imbonerakure, wanaendelea kuwafanyia vitisho raia kwa kuwalazimisha kujiunga, kuunga mkono au kuchangia chama tawala, CNDD-FDD.

Burundi inaendelea kukumbwa na mgogoro wa kisiasa tangu Rais Pierre Nkurunziza atangaze nia yake ya kuwania katika uchaguzi wa urais mwezi Aprili 2015 kwa muhula wa tatu. Alichaguliwa tena mnamo mwezi Julai mwaka huo huo.

Vurugu na ukandamizaji pamoja na mzozo huo vimesababisha vifo vya watu wasiopungua 1,200 na zaidi ya watu 400,000 walitoroka makazi yao kati ya mwezi Aprili 2015 na mwezi Mei 2017, kwa mujibu wa Mahakama ya Jinai ya Kimataifa, ambayo imeanzisha uchunguzi kuhusu hali inayoendelea Burundi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.