Hii ni sensa ya sita tangu uhuru wa nchi ya Kenya iliyopata uhuru wake kutoka kwa Uingereza mwaka 1963, na hufanyika kila baada ya miaka 10, kupata idadi ya watu wanaoishi katika taifa hilo la Afrika Mashariki kwa ajili ya kuisaidia serikali kufanya mipango ya kiuchumi na maendeleo.
Kwa mara ya kwanza, watu wenye jinsia tata, ile ya kiume na kike wanahesabiwa, baada ya kuwepo kwa shinikizo kubwa kutoka kwa wanaharakati na Mahakama kuamuru watambuliwe.
Hata hivyo, zoezi hili pia hutumiwa na wanasiasa ili kuangazia wingi wa wafuasi wao katika ngome zao kwa sababu, siasa za Kenya zimeendelea kuegemea katika mrengo wa ukabila na ukanda.
Rais Uhuru Kenyatta ametoa wito kwa Wakenya kushirikiana na Makarani wanaoshughulikia zoezi hilo ili serikali ifahamu hali zao ya maisha.
"Tungependa kufahamu wewe ni nani, una kitu gani ili kama serikali, tuweze kugawa rasimali tulizopewa na Mwenyezi Mungu kwa usawa ili kumfikia kila mwananchi," alisema rais Kenyatta.
Mbali na majumbani, zoezi hilo linafanyika hospitalini, hotelini na hata katika Uwanja wa Kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi.
Mara ya mwisho kufanyika kwa zoezi hili ilikuwa ni mwaka 2009, na idadi ya Wakenya ilikuwa ni watu Milioni 50.