Pata taarifa kuu
BOBI WINE-YOWERI MUSEVENI-SIASA-AFRIKA

Bobi Wine: Ni wakati wa vijana kuchukua hatamu za uongozi barani Afrika

Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi maarufu kwa jina la Bobi Wine, anasema wakati umefika kwa vijana kuchukua nafasi za kuongoza mataifa ya bara la Afrika.

Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine akihutubia mkutano wa kisiasa katika eneo bunge la Embakasi Mashariki Jijini Nairobi  nchini kenya
Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine akihutubia mkutano wa kisiasa katika eneo bunge la Embakasi Mashariki Jijini Nairobi nchini kenya Twitter/Bobi Wine
Matangazo ya kibiashara

Kyagulanyi ambaye pia ni mwanamuziki, amekuwa ziarani nchini Kenya akikutana na kutoa mihadhara kwa vijana baada ya kualikwa na muungano wa wabunge vijana nchini humo.

Mbunge huyo kijana nchini Uganda, mwenye umri wa miaka 36 amepata nafasi ya kuzungumza na Mwanahabari wa RFI Kiswahili James Shimanyula jijini, aliyetaka kufahamu kwa kina kuhusu harakati zake za kisiasa na maisha yake.

“Muda mwingi wa maisha yangu, nimeishi katika mtaa wa mabanda wa Kamwookya jijini Kampala, nikiwa na mama yangu ambaye alikuwa Muuguzi katika Hospitali ya Mulago,” alisema.

Aidha, amebaini kuwa mama yake alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 15 lakini baba yake alifariki dunia miaka mitatu iliyopita.

Kabla ya kuanza harakati za kisiasa amekuwa mwanamuziki akiimba kuhusu masuala mbalimbali hasa mapenzi, lakini alibadilisha uimbaji wake na kuanza kugusia masuala la kijamii na uongozi bora kwa lengo la kuihamamisha jamii kufahamu haki zao.

“Nimeimba nyimbo nyingi sana, siwezi kukumbuka idadi,”

“Licha ya kuzaliwa katika familia ya kawaida na kuishi Ghetto, nilihakikisha kuwa naupuka umasikini kwa sababu nilikuwa mbunifu,” aliongeza kwa msisitizo.

Kuhusu namna muziki, ulimsaidia, Bobi Wine, amemwambia Mwandishi wetu kuwa, umemsaidia sana na kubadilisha pakuwa maisha yake.

'Muziki umenifanyia mambo mengi sana, umaarufu lakini pia kufahamika na watu,” alisema

Harakati za kisiasa

Kuhusu siasa, mwanasiasa huyo anasema harakati zake ni kuhakikisha kuwa Uganda inajikomboa na uongozi wa rais Yoweri Museveni ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 32.

“Rais Museveni amekuwa rais kwa miaka 32,aliingia madaraka nikiwa na miaka minne tu na kuendelea kwake kusalia madarakani ni kama watu wa zamani wanaopiga pasi nguo zao na kuwasahau watu wa leo,” alisema.

Aidha, amemshtumu rais Museveni kwa kuongoza kwa mkono wa chuma na kudhibiti taasisi kama Bunge na Mahakama.

Mwanasiasa huyo anadai kuwa, kushambuliwa kwake miezi kadhaa iliyopita Kaskazini mwa nchi hiyo ni kutokana na kulemewa na kasi ya wabunge vijana na wenye maoni ya kuibadilisha nchini hiyo.

Baada ya kurejea nyumbani kutoka Marekani alikokwenda kupata matibabu baada ya kuwatuhumu wanajeshi na maafisa wengine wa usalama kwa kumtesa, baada ya kushtumiwa kuchochea wafuasi wake kushambulia msafara wa rais Museveni katika mjini Arua.

Amefunguliwa mashtaka ya uhaini, yanayomsubiri Mahakamani baada ya kupewa dhamana na kuruhusiwa kwenda nje ya nchi kupata matibabu ya afya.

Habari hii ni kutokana na mahojiano baina ya Mwandishi wa RFI Kiswahili, James Shimanyula na Robert Kyagulanyi 'Bobi Wine' yaliyofanyika Jijini Nairobi nchini Kenya.

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.