Pata taarifa kuu
SIASA-TANZANIA-JOHN MAGUFULI

Mtatiro:Ninajiunga CCM kutafuta jukwaa la kufanya siasa

Mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya Chama cha Wananchi CUF, Julius Mtatiro ametangaza kukihama chama hicho, akieleza nia yake ya kujiunga na Chama cha Mapinduzi.

Julius Mtatiro,aliyekuwa mwanasiasa wa upinzani
Julius Mtatiro,aliyekuwa mwanasiasa wa upinzani The Citizen Tanzania
Matangazo ya kibiashara

Kiongozi huyo aliyewahi kuwania ubunge katika majimbo ya Segerea na Ubungo amewaambia wanahabari Mjini Dar es salaam kwamba kwa kipindi cha miaka kumi aliyofanya siasa ametafakari na kuona ni wakati muafaka wa kujiunga na CCM ili kuunga mkono serikali ya Rais John Magufuli.

“Nimejiridhisha kwa nafsi hitaji la nafsi yangu kwamba nijiunge na CCM, nawajulisha watanzania rasmi kuwa nimeanza mipango ya kutekeleza hilo mara moja,”alieleza Mtatiro.

Akiwa mwanasiasa wa upinzani Mtatiro, alijijengea umashuhuri kwa kuwa mkosoaji mkubwa wa serikali akichapisha maandishi yake kwenye mitandao ya kijamii na kwenye magazeti.

Chama alichokuwamo, Mtatiro, CUF, kinakabiliwa na mgogoro usiokwisha kwa miaka miwili sasa tangu Prosefa Ibrahim Lipumba alipotangaza kujizulu, kisha kubatilisha uamuzi wake jambo lililozusha ugomvi usiokwisha ambao unahusisha pande mbili, upande mmoja ukimuunga mkono Profesa Lipumba na mwingine ukimuunga mkono Katibu Mkuu Maalim Seif.

Katibu wa Itikadi na uenezi wa CCM, Humprey Polepole ametumia ukurasa wake wa Twitter kumpongeza Mtatiro kwa kuamua kujiunga na Chama cha mapinduzi.

Hata hivyo, Mbunge wa Malindi Visiwani Zanzibar, Ally Saleh amekosoa hatua ya Mtatiro kukihama chama hicho, akidaia wenye moyo wa kusimamia haki wataendelea kusimama na CUF ambacho ni chama kikuu cha upinzani Visiwani Zanzibar.

Zitto Kabwe, mwanasiasa mwingine wa upinzani na kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo amesema safari bado inaendelea, akisema Mtatiro ameshukia njiani.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2015, viongozi wengi wa upinzani wakiwemo wabunge, madiwani wamekuwa wakivihama vyama vya upinzani na kujiunga na Chama tawala CCM, wakitoa sababu ya kuunga mkono juhudi za serikali ya Rais John Magufuli.

Baadhi ya wabunge waliohama vyama vya upinzani na kujiunga na CCM ni Maulid Mtulia, Mwita Waitara na Julius Kalanga.

Kuhama huko kumepelekea mamilioni ya fedha za walipa kodi wa Tanzania kutumika kugharamia uchaguzi mdogo katika majimbo na kata mbalimbali nchi humo.

Ripoti ya mwandishi wetu, Fredrick Nwaka
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.