Pata taarifa kuu
SUDANI KUSINI-SIASA-USALAMA

Mkataba wa kugawana madaraka waendelea kuchelewa Sudan Kusini

Kutiwa saini kwa mkataba wa awali wa amani kati ya rais wa Sudan Kusini na mpinzani wake Riek Machar kumeahirishwa, baada ya viongozi hao kushindwa kuendelea kuhusu namna ya kugawana madaraka.

Kiongozi wa waasi, Riek Machar (kulia) na rais wa Sudani Kusini, Salva Kiir (kushoto) Mei 9 mwaka 2014.
Kiongozi wa waasi, Riek Machar (kulia) na rais wa Sudani Kusini, Salva Kiir (kushoto) Mei 9 mwaka 2014. REUTERS/Goran Tomasevic
Matangazo ya kibiashara

Ilitarajiwa kuwa, mkataba huo ungetiwa saini jana jijini Khartoum nchini Sudan na baadaye makubaliano rasmi kutiwa saini tarehe 26 mwezi huu.

Ripoti zinasema kuwa, serikali ya Sudan Kusini ndio iliyokataa kuja kusaini mkataba huo baada ya rais Salva Kiir, kuonekana kutokuwa tayari kuwa na Makamu watano wa rais.

Nchi jirani ya Sudan imekuwa mwenyeji wa mazungumzo kati ya wawakilishi wa viongozi wao na wiki hii, walikubaliana namna ya kugawana madaraka.

Pande hasimu Sudan Kusini zimeafiki kugawana madaraka kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa na pande hizo ambapo kwa mujibu wake kiongozi wa waasi nchini humo, Riek Machar atarejeshwa katika wadhifa wa Makamu wa Rais.

Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Al Dierdiry Ahmed,alisema kuwa imeafikiwa kwamba kutakuwepo makamu wanne wa rais; yaani makamu wawili wa rais waliopo hivi sasa pamoja na Riek Machar, na nafasi ya nne ya makamu wa rais atapangiwa mwanamama kutoka kambi ya upinzani.

Itakumbukwa kuwa mrengo wa upinzani nchini Sudan Kusini na serikali ya nchi hiyo walifikia makubaliano katika juhudi za kuhitimisha vita vya wenyewe kwa wenyewe. Vita hivyo vilianza mwaka 2013 baada ya hitilafu za kisiasa kati ya Rais Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake, Machar kusababisha machafuko ya ndani.

Pande mbili hizo hasimu nchini Sudan Kusini zimehusika katika mauaji ya ulipizaji kisasi ambayo yaliibua miganyiko ya kikabila. Makumi ya maelfu ya watu wameuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi kufuatia machafuko hayo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.